Doha, Qatar
Baada ya mshambuliaji wa Brazil, Neymar kuchezewa rafu mara tisa katika mechi na Serbia, kocha wa Brazil, Tite amesema kwamba jambo hilo ni lazima liachwe kama watu wanataka kufurahia soka.
Neymar aliumia enka ya mguu wa kulia Alhamisi iliyopita katika mechi ya kwanza ya Brazil na Serbia kwenye fainali za Kombe la Dunia na kulazmika kutoka uwanjani dakika ya 80 akiwa mwenye huzuni ingawa Brazil ilitoka na ushindi wa mabao 2-0.
Mshambuliaji huyo tegemeo wa Brazil mwenye umri wa miaka 30 aliumia baada ya kuchezewa rafu na Nikola Milenkovic jambo ambalo sasa linaonekana kumkera Tite ambaye atamkosa mchezaji huyo kwenye mechi zote za hatua ya makundi.
“Kama mnataka kufurahia soka muwe makini na rafu, wanaangalia wachezaji fulani wa kuwachezea, hili lina madhara, ni lazima liachwe,” alisema Titte.
Tangu acheze kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, Neymar amechezewa rafu mara 53, idadi ambayo ni kubwa ikiwa mara 11 zaidi ya mchezaji mwingine yeyote.
Katika mechi na Serbia pekee, Neymar amechezewa rafu mara tisa, ikiwa ni mara nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote tangu kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia za Qatar Novemba 20 mwaka huu.
Kwa maumivu aliyoyapata, Neymar ambaye pia ni mshambuliaji wa Paris Saint Germain, daktari wa Brazil alisema atakosa mechi zote za makundi zinazofikia tamati wiki hii. Leo Brazil inacheza na Switzerland, mechi ambayo pia itamkosa beki Danilo.
Mechi za Kombe la Dunia, leo Jumatatu
Kundi G
Cameroon v Serbia
Brazil v Switzerland
Kundi H
Korea Kusini v Ghana
Ureno v Uruguay
