Lusail, Qatar
Lionel Messi Jumamosi hii ameiongoza vyema Argentina kufufua matumaini kwenye fainali za Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mexico na hivyo kuwatoa katika aibu ya kipigo cha mabao 2-1 ilichokipata kwa Saudi Arabia.
Messi alianza kusumbuliwa na wachezaji wa Mexico hasa katika kipindi cha kwanza wakimzibia njia na kumchezea rafu za hapa na pale kabla ya kuwanyamazisha dakika ya 64 alipounasa mpira na kuutuliza vyema kwa guu lake la kushoto kabla ya kufumua shuti la juu la umbali wa mita 20 lililojaa wavuni na kumuacha kipa wa Mexico, Guillermo Ochoa akijaribu kuokoa bila mafanikio
Bao hilo liliwatia ‘uchizi’ mashabiki wa Argentina waliojazana kwenye Uwanja wa Lusail na kulipuka kwa shangwe wakiamini matumaini yao yaliyofifia kwenye fainali za Kombe la Dunia, hatimaye yameibuliwa upya na shujaa na nahodha wao, Messi.
Dakika tatu kabla ya mpira kumalizika, Enzo Fernandez alikamilisha hesabu ya mabao ya Argentina kwa shuti lililojaa wavuni kwa juu na kuwahakikishia Argentina ushindi muhimu ambao pia umethibitisha kile alichosema mshambuliaji wa timu hiyo, Martinez kabla ya mechi hiyo kwamba wangecheza mechi na Mexico kama vile wanacheza mechi yao ya fainali.
Baada ya ushindi huo, Argentina ambayo imejaa matumaini, sasa inasubiri kupata ushindi mwingine katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C dhidi ya Poland ili kujihakikishia kusonga mbele katika hatua ya mtoano kwa kuwa kundi lao bado lipo kimtego.
Poland inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne ikifuatiwa na Argentina yenye pointi tatu sawa na Saudi Arabia na Mexico inashika mkia ikiwa na pointi moja ingawa kimsingi hata Mexico ina nafasi ya kufuzu iwapo itashinda na kuzingatia matokeo ya mechi nyingine yatakavyokuwa.
Matokeo mechi za Jumamosi za Kombe la Dunia
Kundi C
Poland 2- 0 Saudi Arabia
Argentina 2-0 Mexico
Kundi D
Tunisia 0-1 Australia
Ufaransa 2- 1 Denmark
