Lusail, Qatar
Mshambuliaji wa Brazil, Neymar jana Alhamisi usiku aliumia enka wakati timu yake ikitoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Serbia lakini habari njema ni kwamba mchezaji huyo atapona na kuendelea kuiwakilisha timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Qatar.
“Tunaamini Neymar ataendelea kucheza, ataendelea kucheza mechi za Kombe la Dunia,” alisema kocha wa Brazil Tite akiwaambia waandishi wa habari na kuongeza kuwa awali hakuwa anajua chochote kuhusu kuumia kwa mshambuliaji huyo. “Sikuona Neymar kama alikuwa ameumia, na ana uwezo wa kukabiliana na hilo, ni kama vile alinidanganya.
Wakati kocha huyo akisema hivyo, daktari wa timu ya Brazil, Rodrigo Lasmar alisema kwamba watalazimika kusubiri kati ya saa 24 hadi 48 kabla ya kufanyia uchunguzi undani wa maumivu aliyoyapata Neymar kwenye mguu wake wa kulia
“Nadhani atakuwa amejiumiza kwenye enka, na nilimwambia aweke barafu nyingi alipoumia ili apone haraka iwezekanavyo na tuweze kuwa naye kwa asilimia 100 kwenye mechi ijayo, nikifika hotelini nitaenda kuangali anavyoendelea,” alisema daktari huyo mara baada ya mechi ya jana.

Neymar, mshambuliaji bei ghali zaidi duniani, alitoa mchango mkubwa kwa Brazil hadi kupata ushindi wa jana katika mechi hiyo ya kwanza kwa timu hiyo kwenye Kundi G, ndiye aliyempasia Vinicius Jr kabla ya mchezaji huyo kumpasia Richarlison aliyefunga bao la kwanza la Brazil baadaye alionekana akitoka uwanjani akiwa amevua kiatu cha mguu wa kulia ulioumia kwenye enka.
Kuumia kwa Neymar na kulazimika kutoka dakika ya 80 kunawakumbusha mashabiki wa Brazil majanga aliyokumbana nayo mshambuliaji huyo mwaka 2014 kwenye fainali za Kombe la Dunia wakati akipewa nafasi kubwa ya kutamba kwenye fainali hizo zilizofanyika Brazil lakini akapata maumivu ya mgongo na kushindwa kuendelea na michuano hiyo na kuiacha Brazil ikiishia nusu fainali.
Mechi zijazo za Kundi G zitachezwa Jumatatu Novemba 28 kama ifuatavyo… Brazil v Switzerland
Cameroon v Serbia
