Na mwandishi wetu
Kikosi cha cha vinara wa Ligi Kuu NBC, Yanga kimeingia kambini Avic Town Kigamboni leo Alhamisi mapema asubuhi kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbeya City ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi hii.
Timu hiyo imerejea Dar es Salaam jana Jumatano wakitokea mkoani Singida ambako Jumanne walicheza na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Liti na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ameeleza kuwa sababu ya kufikia kambini moja kwa moja ni kutokana na ugumu uliopo kwenye mchezo huo hasa baada ya kushuhudia Mbeya City ikicheza na watani zao Simba na kumaliza mechi kwa sare ya 1-1.
“Baada ya kuangalia mchezo kati ya Mbeya City na Simba, niliona ugumu uliopo kwenye mchezo wetu wa Jumamosi ndiyo maana tumeingia kambini mapema ili kujiandaa na mchezo huo na kurekebisha makosa ambayo yamejitokeza kwenye mchezo uliopita,” alisema Nabi.
Kocha huyo raia wa Tunisia ameeleza kuwa malengo yao ni kuchukua pointi tatu mbele ya Mbeya City lakini ili kutimiza malengo ni lazima wapambane mazoezini ili kutimiza kwa ufanisi mkubwa kile ambacho wamekiandaa mazoezini.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wapo kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi 29 na endapo itaifunga Mbeya City itafikisha pointi 32 baada ya mechi 12 na itakuwa imefikisha mechi 48 bila kufungwa.
Soka Yanga yaiendea kambini Mbeya City
Yanga yaiendea kambini Mbeya City
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
