Na mwandishi wetu
Bondia Twaha Kassim ‘Kiduku’ amesema yuko tayari kumchakaza mpinzani wake katika pambano la kimataifa la kuwania mkanda wa Dunia wa WBF dhidi ya bondia wa Argentina, Hugo Victor katika pambano litakalopigwa wikiendi hii mkoani Morogoro.
Akizungumza leo bondia huyo alisema amejipanga vizuri na anamuheshimu mpinzani wake akijua wazi hapaswi kumbeza ila atahakikisha hawaangushi mashabiki wake.
“Nimefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha nawapa raha mashabiki wangu, naomba mjitokeze kwa wingi kwenye Uwanja wa Jamhuri na mimi sitawaangusha,”alisema Kiduku.
Kiduku amekuwa kwenye kiwango bora tangu mwaka jana ambapo katika mapambano matatu aliyocheza mfululizo hajapoteza hata moja.
Mara ya mwisho alicheza na bondia kutoka Misri, Abdo Khaled na kushinda katika pambano hilo lililochezwa Machi mwaka huu mkoani Mtwara.
Pia mbali na pambano la Kiduku, kutakuwa na pambano litakalowahusisha mabondia Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ dhidi ya Limbani Lano kutoka Jeshi la Malawi badala ya Mbiya Kanku wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo aliyetangazwa awali.
Mbabe anatakiwa kuwathibitishia Watanzania kuwa sasa amerudi upya baada ya kufanya vibaya katika pambano lake la mwisho la kimataifa dhidi ya bondia kutoka Congo, Erick Katompa.
Mbabe alisema amekuwa na bahati mbaya ya kubadilishiwa mabondia dakika za mwishoni na mwaka jana ilitokea kama ilivyo sasa lakini sasa hana hofu amejiandaa vya kutosha na yuko tayari kupambana na yeyote.
Mapambano mengine ya utangulizi yatakuwa ni kati ya Karim Mandonga dhidi ya Said Mbelwa, Issa Maneva dhidi ya Oscar Goba, Magambo Christopher dhidi ya Juma Misumari na mabondia wengine.
Ngumi Kiduku atamba kumchakaza Muargentina
Kiduku atamba kumchakaza Muargentina
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
