Na mwandishi wetu, Mbeya
Mbeya City leo Jumatano imeendelea kudhihirisha jeuri yake kwa Simba kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya baada ya kuilazimisha sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC.
Mechi ya leo ni ishara nyingine kwamba Uwanja wa Sokoine ni mgumu kwa Simba kwani timu hizo zilipokutana katika uwanja huo msimu uliopita, Simba ililala kwa bao 1-0 japo baadaye ililipa kisasi timu hizo ziliporudiana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kwa ushindi wa mabao 3-0.
Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 14 lililofungwa na Mzamiru Yassin kwa shuti la chinichini la mguu wa kushoto lililomshinda kipa wa Mbeya City, Lameck Kanyonga. Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Clatous Chama aliyempasia Bocco ambaye aliunganisha pasi ya kisigino kwa mfungaji.
Mbeya City walisawazisha bao hilo dakika ya 78 mfungaji akiwa Tariq Seif ambaye aliinasa krosi ya Awadh Juma iliyotokea upande wa kushoto ambapo Seif alifumua shuti la chinichini lililowapita mabeki wa Simba na kipa wao, Aishi Manula. Hilo lilikiwa ni bao la nne kwa Seif msimu huu.
Simba pamoja na kupata bao hilo ilifanya mashambulizi katika dakika ya 55, Kibu Dennis aliufumania mpira na kufumua shuti la mbali ambalo kipa wa Mbeya City aliokoa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 73 tena, Shomari Kapombe alipiga mpira wa adhabu uliotokea upande wa kulia na Joash Onyango akaunganisha kwa kichwa lakini hakuweza kuipatia Simba bao.
Dakika tatu baadaye Mbeya City walijibu mapigo baada ya Gapar Mwaipasi akiwa upande wa kushoto kufumua shuti ambalo lilitoka nje sentimita chache lakini Manula akaufuata mpira huo kwa tahadhari na kuudaka na mwamuzi akaipa Mbeya City kona ambayo haikuzaa matunda.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa inazidi kuipa ahueni Yanga katika mbio za kuliwania taji la ligi hiyo ikiwa imeachwa kwa pointi mbili huku Yanga ikiwa imecheza mechi 11 na Simba 13 sawa na Azam ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 29 lakini imezidiwa na Yanga kwa mabao ya kufunga.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo, Singida Big Stars ilifanikiwa kutoka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya KMC.
Soka Mbeya City yaivimbia Simba
Mbeya City yaivimbia Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
