Doha, Qatar
Kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong aliyekuwa akisakwa na Man United hatimaye ametangaza kwamba anataka kuichezea Barcelona kwa miaka 10 ijayo licha ya utata uliowahi kuibuka kati yake na bodi ya klabu hiyo.
Katika majira ya kiangazi De Jong alikuwa gumzo akiwaniwa na Man United, mpango ambao haukufanikiwa licha ya kocha wa Man United, Erik ten Hag kusema kwamba angependa kuungana na mchezaji huyo ambaye pia anatokea Uholanzi kama ilivyo kwa kocha huyo.
De Jong ni kati ya wachezaji wenye namba ya uhakika katika kikosi cha Barca chini ya kocha Xavi Hernandez ingawa hadithi yake na Man United imeendelea kuwa mjadala kwa kipindi kirefu hata baada ya msimu wa ligi za Ulaya kuanza.
“Nina raha sana kuwa Barcelona, ninapocheza najisikia vizuri na kuhusu maisha nafurahia kuwa pale, maisha yako safi, najiona nikiwa Barcelona kwa muda mrefu kadri itakavyowezekana, ni matumaini yangu kuwa pale kwa miaka mingine minane au 10,” alisema De Jong jana Jumatatu mjini Doha, Qatar, muda mfupi kabla ya mechi kati ya Uholanzi na Senegal ambayo Uholanzi ilishinda kwa mabao 2-0.
Barca iliwahi kufanya mazungumzo na Man United wakati Man United ikimtaka mchezaji huyo na habari za ndani zilidai kwamba De Jong kama angekataa kupunguziwa mshahara na kusogezwa mbele mpango wowote wa nyongeza katika pato lake wakati wa janga la korona, klabu hiyo ingelazimika kufikira mpango wa kumfanyia uhamisho.
Pia ilidaiwa kwamba vigogo wa Barca walifikia hatua ya kuwaandikia barua wawakilishi wa De Jong na kuhoji uhalali wa mkataba wa mchezaji huyo na klabu hiyo ambao ulisainiwa na uongozi uliopita chini ya aliyekuwa rais wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu.
Akizungumzia kukosekana usiri katika mkataba na maslahi yake, De Jong alisema, “nawalaumu hawa watu lakini sina la kuwafanya, ndio hao ni Barca kwani ndio wanaosimamia klabu lakini huwa siwaoni nikiwa klabuni, sina mahusiano nao yoyote katika maisha yangu ya kila siku.”
“Kuna siku gazeti lilichapisha undani wa mkataba wangu, si mimi niliyetoa hiyo habari na aliyefanya hivyo anayejua ni upande wa pili, na hiyo ni klabu iliyofanya hivyo,” alisema De Jong ambaye kwa sasa yuko Qatar akiiwakilisha Uholanzi kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Kimataifa De Jong ataka miaka 10 Barca
De Jong ataka miaka 10 Barca
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
