Doha, Qatar
England, Wales na mataifa mengine ya Ulaya hawatavaa tena vitambaa maalum vyenye ujumbe wa umoja na mapenzi kwa wote kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa sababu ya hofu ya wachezaji wao kupewa kadi.
Manahodha wakiwamo Harry Kane wa England na Gareth Bale wa Wales tangu jana ilielezwa kuwa walipanga kuvaa vitambaa vya unahodha katika mechi zao vyenye ujumbe wa kuhamasisha usawa na umoja na ushirikishwaji kwa watu wote licha ya Fifa kupiga marufuku jambo hilo.
Taarifa ya pamoja kutoka vyama saba vya soka vya Ulaya ilieleza kuwa hawatokuwa tayari kuwaweka wachezaji wao katika mazingira ambayo wanaweza kujikuta wakiadhibiwa na kueleza kuwa wamechukizwa na uamuzi huo wa Fifa.
Kwa mantiki hiyo, England ambayo leo inaumana na Iran itajitupa uwanjani bila ya kuwa na ujumbe huo kama ilivyo kwa Wales inayoumana na Marekani, badala yake timu hizo sasa zitalazimika kufuata maelekezo ya Fifa ambao wametoa vitambaa vyenye ujumbe tofauti.
“Fifa wamekuwa wazi kwamba watatoa adhabu kwa manahodha wetu wakivaa vitambaa vyenye ujumbe huo uwanjani, awali tulijiandaa kwa faini kwa kosa la kuvunja kanuni na tulikuwa na dhamira ya dhati ya kuvaa vitambaa hivyo lakini hatuwezi kuwaweka wachezaji wetu katika mazingira ambayo wanaweza kupewa kadi au hata kujikuta wakitolewa nje,” ilifafanua taarifa hiyo.
England wataanza kuumana na Iran na baadaye Wales na Marekani katika mechi za Kundi A na sasa manahodha hao watavaa vitambaa vyenye ujumbe unaopinga vitendo vya ubaguzi ambayo ni maelekezo ya Fifa kwa timu zote.
Inadaiwa kwamba mataifa hayo pamoja na kukerwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Qatar ikiwamo unyonyaji unaodaiwa kufanywa kwa wahamiaji wanaofanya kazi nchini humo kubwa linalowakera ni namna nchi hiyo isivyothamini haki za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja ambayo ni kosa la jinai.
Kimataifa Kina Kane watii agizo la Fifa
Kina Kane watii agizo la Fifa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
