Doha, Qatar
Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Karim Benzema anazikosa fainali za Kombe la Dunia baada ya kuumia misuli ya paja la mguu wa kulia wakati akifanya mazoezi na timu ya Ufaransa jana Jumamosi mjini Doha.
Benzema ni mmoja wa washambuliaji waliotarajiwa kung’ara katika fainali za Kombe la Dunia za Qatar akiwa ametoka kuiwezesha Real Madrid kubeba taji la Ligi Kuu Hispania na lile la Mabingwa Ulaya na ndiye kinara wa Ballon d’Or, kukosekana kwake kunakuwa pigo kubwa kwa timu ya Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia.
Shirikisho la Soka Ufaransa limethibitisha kuumia kwa mchezaji huyo wakati akiwa mazoezini baada ya kukimbia kwa kasi wakati akiwa katika hatua za mwisho za mazoezi na baada ya vipimo ilibainika amepata majeraha ambayo yatahitaji wiki tatu hadi kupona.
Fainali za Kombe la Dunia ambazo zinaanza leo Jumapili kwa wenyeji Qatar kuumana na Ecuador na kufikia ukomo Desemba 18, zitamkosa mshindi huyo wa Ballon d’Or ikiwa ni mara ya kwanza kwa mshindi wa tuzo hizo kukosekana kwenye michuano tangu mwaka 1978.
Ufaransa itaingia uwanjani kucheza mechi yake ya kwanza ya kulitetea taji hilo keshokutwa Jumanne dhidi ya Australia na kwa mujibu wa kanuni za Fifa, Ufaransa itakuwa na muda wa saa 24 kabla ya kucheza mechi yao ya kwanza ili kumtangaza mchezaji wa kuchukua nafasi ya Benzema.
Washambuliaji wengine wa Ufaransa ukiacha Benzema ni Kylian Mbappe pamoja na Antoine Griezmann, Olivier Giroud, Marcus Thuram na Ousmane Dembele.
“Nimesikitishwa na kilichomkuta Karim, ambaye fainali hizi za Kombe la Dunia zilikuwa ni lengo lake kuu, licha ya pigo hili jipya kwa timu ya Ufaransa bado nina imani kubwa na kundi la wachezaji wangu, tutafanya kila kitu kukabiliana na changamoto kubwa inayotusubiri,” alisema kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps katika taarifa yake.
Akizungumzia kuumia kwake na kuzikosa fainali hizo, Benzema alisema, “Sijawahi kukata tamaa katika maisha yangu lakini leo (jana) nalazimika kuifikiria timu kama ambavyo nimekuwa nikifanya siku zote, sababu zinaniambia nimpe nafasi yangu mtu mwingine ambaye ataweza kuisaidia timu kuwa na michuano mizuri ya Kombe la Dunia,” asanteni kwa kuniunga mkono.
Kabla ya Benzema, Ufaransa pia ilipata pigo baada ya mshambuliaji wa RB Leipzig, Christopher Nkunku kuumia pamoja na beki wa kati wa PSG, Presnel Kimpembe ambao nafasi zao wamepewa, Randal Kolo Muani wa Eintracht Frankfurt ya Ujerumani na Axel Disasi wa Monaco ya Ufaransa.
Ufaransa tayari ilikuwa katika wakati mgumu kwa kuwakosa viungo wake tegemeo, Paul Pogba na N’Golo Kante, ambao ni majeruhi. Miaka minne iliyopita wachezaji hao walitoa mchango mkubwa kwa timu hiyo hadi kubeba Kombe la Dunia nchini Urusi.
Kwa Benzema ni kama vile ana bahati mbaya na fainali za Kombe la Dunia, mwaka 2014 alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo lakini akazikosa fainali za 2018 ambazo Ufaransa ilibeba taji baada ya kusimamishwa akihusishwa na kashfa ya mkanda wa ngono pamoja na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Mathieu Valbuena.
Kimataifa Majeruhi Benzema akosa Kombe la Dunia
Majeruhi Benzema akosa Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
