Doha, Qatar
Kama ulitarajia kushuhudia mechi za Kombe la Dunia ukiwa na bia mkononi sahau, katika fainali za mwaka huu zitakazofanyika Qatar kuanzia keshokutwa Jumapili, uuzaji wa bia kwenye viwanja vinane vitakavyotumika kwa mechi za fainali hizo umepigwa marufuku.
Uamuzi huo tofauti umekuja baada ya Fifa kuamua kubadili sera ikiwa ni siku mbili kabla ya kuanza kwa fainali hizo kwani hapo kabla, uuzaji wa bia uliruhusiwa katika baadhi ya maeneo ya karibu na viwanja licha ya marufuku iliyopo siku zote katika nchi ya kiislam.
Na ingawa kinywaji hicho kimepigwa marufuku viwanjani lakini kwa baadhi ya maeneo marufuku hiyo haitokuwapo na hivyo bia zitauzwa. Kampuni ya Budweiser, ambao ni kati ya wadhamini wakubwa wa Fifa, ni kampuni inayozalisha bia na imepewa haki kuuza bia katika fainali hizo.
“Kufuatia mazungumzo baina ya wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia na Fifa, uamuzi umefikiwa wa kuuza kinywaji hicho katika maeneo mengine ya mashabiki na yenye leseni maalum na kuzuia uuzaji wa kinywaji hicho kwenye viwanja vinane vitakavyotumika kwa mechi za michuano hiyo,” ilieleza taarifa hiyo ya Fifa.
“Hakuna zuio la uuzaji wa kinywaji cha Bud Zero ambacho kitapatikana kwenye viwanja vyote vya Qatar vitakavyotumika kwenye fainali za Kombe la Dunia. Wenyeji Qatar na Fifa wataendelea kuhakikisha viwanja na mazingira jirani yanatoa fursa kwa mashabiki wote kufurahia michuano kwa amani na utulivu,” ilifafanua taarifa hiyo.
Chama cha Mashabiki wa Soka (FSA) kimelalamikia muda wa uamuzi huo wa kuzuia uuzwaji wa bia kwa mashabiki walio wengi kwa sababu kuna mashabiki wanaopenda kuwa na bia wakati mechi ikiendelea lakini jambo baya ni uamuzi huo kufikiwa katika hatua za mwisho.
Wenyeji wa michuano hiyo, timu ya Qatar itacheza mechi yake ya kwanza Jumapili dhidi ya timu ya Ecuador.
Kimataifa Bia marufuku viwanjani Qatar
Bia marufuku viwanjani Qatar
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
