Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski amefungiwa mechi tatu kwa kosa la kumuonyesha mwamuzi ishara mbaya baada ya kupewa kadi nyekundu katika mechi ya La Liga dhidi ya Osasuna.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumanne iliyopita na Barca kuibuka na ushindi wa 2-1, mchezaji huyo alitolewa baada ya kupewa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu, wakati akitoka uwanjani alishika pua yake na kumuonyeshea mwamuzi wa mechi hiyo, Jesus Gil Manzano, kitendo kilichotafsiriwa na Shirikisho la Soka Hispania (RFEF) kuwa ni ishara ya kumkosea mtu heshima na ujeuri.
Lewandowski akijitetea alidai kuwa ishara hiyo hakuielekeza kwa mwamuzi kama RFEF walivyotafsiri badala yake ilikuwa ni kwa kocha wake Xavi Hernandez kutokana na mazungumzo baina yao mapema mwezi huu lakini shirikisho hilo halikuyapa umuhimu maelezo ya mchezaji huyo.
Mshambuliaji huyo hadi sasa ameifungia Barca mabao 18 katika michuano yote msimu huu, na kwa adhabu hiyo atakosa mechi dhidi ya Espanyol ambayo imepangwa kupigwa Desemba 31 na baada ya hapo atazikosa mechi dhidi ya Atletico Madrid na Real Betis kwa kuwa mechi za La Liga kwa sasa zimesimama kwa wiki sita kupisha fainali za Kombe la Dunia.
Hii ni mara ya pili kwa Lewandowski kupewa kadi nyekundu katika maisha yake ya soka la hadhi ya juu, aliwahi kukutana na hali hiyo mwaka 2013 wakati akiichezea Borussia Dortmund. Kwa sasa mchezaji huyo yupo Qatar akiiwakilisha Poland kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Kimataifa Lewandowski afungiwa mechi 3
Lewandowski afungiwa mechi 3
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
