Paris, Ufaransa
Shirikisho la Soka Ufaransa limethibitisha kwamba mshambuliaji wa timu hiyo, Christopher Nkunku atazikosa fainali za Kombe la Dunia baada ya kuumia wakati akiwa mazoezini jana Jumann na tayari nafasi yake amepewa mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Randal Kolo Muanie.
Nkunku anayeichezea klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani aliumia goti la kushoto na hivyo Ufaransa itamkosa mchezaji huyo wakati huu ikijiandaa kulitetea taji hilo ililolibeba mwaka 2018 kwa kucheza mechi yake ya kwanza Novemba 22 dhidi ya Australia. Kanuni za Fifa zinaruhusu timu kubadili mchezaji saa 24 kabla ya kucheza mechi ya kwanza.
Kutokana na hali hiyo, Shirikisho la Soka Ufaransa limesema kwamba nafasi ya Nkunku itajazwa mara baada ya timu ya madaktari wa timu hiyo kukamilisha ripoti yake na kupelekwa Fifa.
Juzi Jumatatu Ufaransa iliwaita katika timu hiyo mshambuliaji Marcus Thuram anayeichezea Borussia Monchengladbach na beki wa Monaco, Axel Disasi ambaye aliitwa baada ya beki wa kati ya PSG, Presnel Kimpembe kutangaza kujitoa kwenye timu hiyo kutokana na matatizo ya misuli.
Katika kikosi cha Ufaransa kinachonolewa na kocha Didier Deschamp, Nkunku alitegemewa kupangwa katika mechi za Ufaransa nyuma ya washambuliaji Karim Benzema na Kylian Mbappe na hapana shaka kazi hiyo sasa itafanywa na Muanie ambaye ameifungia Frankf.urt mabao manane katka mechi 23 za msimu huu.
Kimataifa Majeruhi Nkunku apata mrithi Ufaransa
Majeruhi Nkunku apata mrithi Ufaransa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
