Tehran, Iran
Kocha wa timu ya Taifa ya Iran, Carlos Queiroz amesema kwamba wachezaji wake wana uhuru wa kufanya maandamano ya kutetea haki za wanawake nchini kwao wakati huu wakiwa Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Maandamano yamekuwa yakifanyika nchini Iran takriban miezi miwili sasa baada ya kifo cha Mahsa Amini, msichana wa miaka 22 ambaye alikamatwa na kufungwa na polisi wanaosimamia maadili nchini Iran kwa kosa la kwenda kinyume na sheria inayomtaka kujihifadhi ikiwamo kufunika kichwa chake.
Viongozi wa Iran wamekuwa wakidai kwamba maandamano hayo ni vurugu ambazo zinahamasishwa na mataifa ya nje ambayo ni maadui wa Iran.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari inadaiwa kuwa waandamanaji zaidi ya 100 wameuliwa kutokana na kampeni iliyoendeshwa na maofisa usalama kukabiliana na waandamanaji hao hadi sasa huku miongoni mwa wanaodaiwa kuuawa wakiwamo watoto 43 na wanawake 25.
Kocha wa Iran, Queiroz ambaye pia amewahi kuzinoa timu za Man United, Real Madrid na timu ya Taifa ya Ureno, pamoja na kuruhusu maandamano hayo, hata hivyo amesema kila atakayetaka kufanya maandamano hayo lazima azingatie kanuni zinazotawala fainali za Kombe la Dunia.
“Wachezaji wapo huru kuandamana kama wanataka kama watakuwa katika nchi nyingine yoyote ila tu wakubaliane na kanuni za Kombe la Dunia pamoja na na taratibu za mchezo wa soka,” alisema.
“Pia unaweza kueleza dukuduku lako uwanjani katika mechi ya soka lakini hapo hapo wachezaji wanatakiwa kuwa na jambo moja katika akili zao, nalo ni kufuzu raundi ya pili,” alisema.
Iran ambayo imepangwa Kundi B katika fainali hizo itaanza mechi yake dhidi y England. Jumatatu kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa.
Kimataifa Kocha Iran aruhusu wachezaji kuandamana Qatar
Kocha Iran aruhusu wachezaji kuandamana Qatar
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
