Na mwandishi wetu
Kikosi cha timu ya Simba Queens kinatarajiwa kuwasili nchini usiku wa kuamkia kesho kikitokea nchini Morocco kilipokuwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake iliyomalizika juzi.
Queens waliomaliza kwenye nafasi ya nne ya michuano hiyo iliyodumu kwa takriban wiki tatu, kilianza safari yake ya kurejea nchini juzi kwa kupitia nchini Uturuki ambapo walilala hapo kabla ya leo usiku kuendelea na safari.
Timu hiyo imeshiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo iliyoanza msimu uliopita na kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali, inarejea nchini ikiwa imejipatia kitita cha Dola za Marekani 200,000 (zaidi ya Sh milioni 460) kama zawadi kwa kushika nafasi ya nne.
Queens inayonolewa na Charles Lukula raia wa Uganda ilifungwa bao 1-0 kwenye nusu fainali na waliokuwa mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kabla ya kufungwa idadi hiyo hiyo tena na Bayelsa Queens ya Nigeria kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.
Katika michuano hiyo, wenyeji AS FAR walitawazwa mabingwa wapya baada ya kuitungua Mamelodi mabao 4-0 na kuzoa kitita cha Dola za Marekani 400,000 huku Mamelodi walioshika nafasi ya pili wakijinyakulia Dola 250,000.
Lukula amewashukuru mashabiki wa Simba kwa kuwaunga mkono muda wote wa michuano hiyo na upendo waliokuwa wakiwaonesha, akisema kuwa wamefarijika mno na hawatawaangusha wakati mwingine watakaposhiriki michuano hiyo.
Soka Simba Queens yarejea Dar
Simba Queens yarejea Dar
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
