London, England
Ni kishindo cha Arsenal. Ligi Kuu England (EPL) imesimama kupisha fainali za Kombe la Dunia Arsenal ikiwa kinara kwa tofauti ya pointi tano, ni namba zinazoonyesha kwamba dhamira ya kocha Mikel Arteta kulibeba taji msimu huu zinakwenda vizuri.
Arsenal ilifunga hesabu zake juzi Jumamosi kwa ushindi wa ugenini wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves na kufikisha pointi 37 ikineemeka kwa mabao ya Martin Odegard katika dakika za 54 na 75 na kupata ushindi ambao unawafanya wachezaji wa timu hiyo wanaoziwakilisha nchi zao kwenye fainali za Kombe la Dunia kwenda Qatar wakiwa na amani.
Ushindi huo umekuja wakati ambao wapinzani wao katika mbio hizo, Man City wameingia katika kipindi kigumu kidogo kwani wanakwenda mapumziko baada ya Jumamosi kuchapwa mabao 2-1 na Brentford tena wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Ni vigumu kusema moja kwa moja kwamba Arsena itatwaa ubingwa wa EPL msimu huu wa 2022/23 ambao bado haujafika hata nusu kwani timu zote zimecheza kati ya mechi 14 na 15 lakini si vibaya kusema kwamba kwa hali ilivyo sasa, kasi ya Arsenal inatoa matumaini ya kulibeba taji hilo.
Pengine hakuna ambaye alitarajia timu hiyo ingekuwa mahali ilipo msimu huu hadi sasa na hivyo kufika hapo ilipo ni ishara moja kubwa kwamba Arsenal hii imepania kufanya makubwa msimu huu.
Jambo jingine ambalo linazidisha matumaini hayo ni namna ambavyo vigogo walizoeleka wa ligi hiyo, Liverpool, Man United na Chelsea wanavyokwenda mwendo wa kuchechemea.
Ukiacha Man City ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa imeachwa na Arsenal kwa tofauti ya pointi tano, Man United inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 23 tofauti ya pointi 14 kwa Arsenal, Liverpool ni ya sita ikiwa na pointi 22 na Chelsea ni ya nane ikiwa na pointi 21.
Kwa ligi ilipofika timu zilizo katika nne bora au Top Four, ukiacha Man City, maadui wengine wa Arsenal ni Newcastle na Tottenham, si timu za kubeza lakini mbali na mazingira yalivyo sasa kwenye msimamo wa EPL kuibeba Arsenal dhidi ya timu hizo, historia pia inaibeba Arsenal kwani hizo si timu shindani zilizoeleka katika EPL kama ilivyo kwa Man United, Liverpool na Chelsea.
Pamoja na matumaini yote hayo bado si sahihi kusema moja kwa moja kwamba Arsenal ni bingwa kwani bado kuna kazi ngumu mbele yao mara baada ya fainali za Kombe la Dunia na mechi za EPL kuanza tena kuanzia Desemba 26 ingawa mashabiki wana kila sababu ya kufurahia mwenendo wa timu yao na kujipa matumaini.
Matokeo ya mechi za EPL mwishoni mwa wiki ni kama ifuatavyo…
Man City 1-2 Brentford
Bournemouth 3-0 Everton
Liverpool 3-1 Southampton
Nottm Forest 1-0 Crystal Palace
Tottenham 4-3 Leeds
West Ham 0-2 Leicester
Newcastle 1-0 Chelsea
Wolves 0-2 Arsenal
Brighton 1-2 Aston Villa
Fulham 1-2 Man Utd
Kimataifa Kishindo cha Arsenal EPL
Kishindo cha Arsenal EPL
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
