Anderlecht, Ubelgiji
Kocha wa timu ya Taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez amesema kwamba mshambuliaji Romelu Lukaku ni lazima awe fiti kiasi cha kutosha kuiwakilisha timu hiyo kwenye Kombe la Dunia vinginevyo hatokuwa na nafasi.
Martinez anatarajia kutaja kikosi chake baadaye leo Alhamisi huku nafasi ya mshambuliaji huyo wa Inter Milan ya Italia ikiwa njia panda kwani haijulikani kama atachaguliwa au la hasa baada ya klabu yake kumuweka kando kutokana na matatizo ya misuli yanayomuandama.
“Uamuzi utafikiwa muda mfupi kabla ya kutangaza majina, utazingatia mechi za kwanza za hatua ya makundi kama atakuwa na uwezo wa kushiriki katika moja ya mechi hizo, huyo ni mchezaji ambaye tutamhitaji kwenye timu yetu kama hawezi hatokuwa na nafasi,” alisema Martinez.
Lukaku amekuwa akifanyiwa majaribio ya mara kwa mara na timu ya madaktari wa Ubelgiji hasa kwa kuwa tangu Agosti amecheza mechi mbili tu za Inter ambazo zote ameingia kipindi cha pili.
Kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza kutimua vumbi Novemba 20, Ubelgiji itaanza kampeni yake Novemba 23 dhidi ya Canada na kufuatiwa na mechi dhidi ya Morocco siku nne baadaye kabla ya kumalizia mechi za makundi dhidi ya Croatia itakayopigwa Desemba Mosi.
“Tumeona dalili njema lakini tunalazimika kusubiri hadi muda mfupi kabla ya kutangaza kikosi ili tuwe na muda wa kutosha kufanya maamuzi,” aliongeza Martinez.
Kimataifa Lukaku njia panda Kombe la Dunia
Lukaku njia panda Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
