
Na mwandishi wetu
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda ameeleza namna gani mambo yake yamevurugika baada ya taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu kumfungia mechi tatu kiungo wake, Clatous Chama.
Chama amefungiwa kutoichezea timu hiyo mechi za Ligi Kuu pamoja na faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kutosalimiana na wachezaji wa Yanga katika pambano la watani wa jadi lililopigwa Oktoba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mgunda ameeleza kuwa maamuzi hayo kwa kiasi kikubwa yamevuruga malengo yake katika mechi hizo tatu ambazo watacheza ndani ya mwezi huu wa Novemba na tayari leo wameumana na Singida Big na kutoka sare ya bao 1-1.
“Chama ni mchezaji wangu tegemezi kwenye kikosi changu, kumkosa katika mechi tatu mfululizo ni pigo kubwa, ni sawa na kuvuruga mipango yangu ambayo nimejiwekea ndani ya mwezi huu,” alisema kocha Mgunda.
Kocha huyo amefafanua kuwa hakatai mchezaji huyo kuadhibiwa lakini kitendo cha adhabu hiyo kuchelewa kutolewa ndiyo kimemkwaza ukizingatia mwezi huu wanakabiliwa na mechi sita ngumu na zote wamepania kushinda.
Alisema pamoja na upana wa kikosi chake lakini uwepo wa Chama ni kitu muhimu katika kipindi hiki ambacho wanapambania kuhakikisha wanarudi kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kushinda kila mchezo uliopo mbele yao.
Mgunda pia alifunguka kuwa haifundishi kazi kamati husika bali anafanya hivyo kwa manufaa ya timu yake ili kutimiza malengo ambayo wamejiwekea ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
Katika adhabu hiyo iliyotolewa jana pia ilimkumba kiungo wa Yanga, Stephanie Aziz Ki kwa kufanya kosa kama hilo.
