Na mwandishi wetu
Stephane Aziz Ki leo Jumatano ameendelea kudhihirisha thamani yake ndani ya kikosi cha Yanga baada ya kufunga bao pekee muhimu dhidi ya Club Africain ya Tunisia na kuiwezesha Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hii inakuwa mara ya pili katika siku za karibuni kwa Aziz Ki kuifungia timu yake bao muhimu na katika mechi muhimu, alifanya hivyo dhidi ya mahasimu wao Simba alipofunga bao la mpira wa adhabu na kuiwezesha Yanga kutoka sare ya bao 1-1, sare ambayo imeendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo katika Ligi Kuu NBC tangu msimu uliopita.
Katika mechi ya leo bao la Aziz Ki lilipatikana katika dakika ya 79 kwa mpira ulioanzia kwa krosi iliyochongwa na Salum Aboubakar na kumkuta Fiston Mayele ambaye alimuunganishia Azizi Ki pasi ya kichwa ambaye bila ajili akafumua shuti la mguu wa kushoto lililojaa wavuni.
Kwa ushindi huo Yanga sasa inasonga mbele katika michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana wiki moja iliyopita katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ukiachana na bao hilo, Yanga tangu awali ilionyesha imedhamiria kupata ushindi kutokana na mashambulizi kadhaa iliyofanya kwa wapinzani wao licha ya mashambulizi hayo kutozaa bao.
Mfano dakika ya 25 Fei Toto alimpa pasi ya kisigino Kibwana Shomari ambaye alifumua shuti na kama si umahiri wa kipa wa Africain, Yanga ingeweza kupata bao la mapema.
Africain nao mara kadhaa walilisakama lango la Yanga lakini umahiri wa safu ya ulinzi ya timu hiyo iliyoongozwa vyema na kipa Djugui Diarra ambaye alikuwa akitoa maelekezo ya mara kwa mara kwa wachezaji wake ulikuwa kikwazo kwa wenyeji kupata bao.
Ushindi wa leo wa Yanga umekuja wakati baadhi ya mashabiki wa Yanga walishakata tamaa kutokana na matokeo ya awali wakiamini isingewezekana kwa timu yao kusonga mbele baada ya kukubali sare ya kutofungana kwenye uwanja wake wa nyumbani huku Africain wakionekana kucheza mechi hiyo ya awali kwa umakini mkubwa na mbinu nyingi.
Awali baadhi ya mashabiki pia walionekana kushangazwa na uamuzi wa kocha Nabi kumuweka benchi Aziz Ki na hatimaye kumuingiza kipindi cha pili akichukua nafasi ya Khalid Aucho, mabadiliko ambayo yameonyesha jinsi mbinu ya kocha huyo kumuanzisha benchi mchezaji huyo ilivyokuwa na maana kwa kuipa Yanga ushindi.
Kimataifa Yanga yapendeza Tunisia
Yanga yapendeza Tunisia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
