Na mwandishi wetu
Kikosi cha Yanga kimetua salama nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain kikiwa na morali ya kutosha kupata matokeo ugenini.
Meneja wa Yanga, Walter Harrison ameeleza kwamba hali ya kikosi kipo vizuri na moja kwa moja baada ya kutua Mjini Tunis, kikosi hicho kimeelekea katika Mji wa Sousse kwa ajili ya kuweka kambi ya siku mbili ya kujiweka sawa.
Harrison alieleza kuwa wameamua kwenda Sousse sababu hawakutaka kukaa karibu na jiji la wapinzani wao, Tunis, pia wakiamini Sousse ni sehemu tulivu kwa ajili ya kupumzika na kuweka umakini juu ya mechi hiyo ya kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
“Tunashukuru Mungu tumesafiri salama mpaka hapa, hali ya kikosi kiujumla iko vizuri, wachezaji wako vizuri kabisa na morali iko juu sana kuona jinsi gani tunaweza kupata matokeo, tunahitaji kuwa na hali hii mpaka siku ya mchezo na endapo ikiwa hivi tunaamini tunaweza kufanya jambo ambalo wengi hawalitarajii, naamini tunaweza kurudi na ushindi.
“Tumeamua kwenda Sousse kwa ajili ya utulivu na umakini wa mchezo na tutakaa siku mbili ambapo leo (jana) tutafanya mazoezi mepesi kabla ya kurejea Tunis kwa ajili ya mchezo wa Jumatano na kila kitu kipo sawa,” alisema Harrison.
Yanga hata hivyo katika mechi hiyo itamkosa beki wake wa kulia, Djuma Shaban kutokana na majeraha ya nyama za paja aliyoyapata Jumatano iliyopita walipoumana na Africain kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika mchezo ulioisha kwa suluhu.
“Alipata majeraha kwenye mechi iliyopita na alitolewa kutokana na nyama za paja zilimsumbua kwa hiyo kiufundi kocha (Nasreddine Nabi) anajua nini atafanya lakini kwa upana wa kikosi naamini tutakuwa na mbadala wake ambaye atatoa mchango mkubwa na kutuwakilisha vizuri Wananchi,” alisema Harrison.
Yanga ilianza safari yake juzi kupitia Dubai kabla ya jana kutua Tunis, baada ya kambi yao ya siku mbili watarejea Tunis siku moja kabla ya mchezo kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Hammedi Agrebi itakapopigwa mechi hiyo.
Katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu, Yanga itahitaji ushindi au sare ya mabao ili kusonga mbele na kama ikiisha kwa suluhu, mikwaju ya penalti itaamua mshindi.
LigiKuu Yanga iliyojaa morali yatua Tunisia
Yanga iliyojaa morali yatua Tunisia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
