Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube ameibuka na kutoa ya moyoni ni namna gani alikuwa anapitia kipindi kigumu kabla ya kuanza kufunga mabao tena hivi karibuni kwenye mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu ya NBC Bara.
Dube ambaye alikuwa majeruhi kwa kipindi kirefu msimu uliopita, msimu huu ulipoanza hakuonesha makali yake zaidi ya kufunga bao moja kwenye mechi ya ufunguzi na kisha kurejea kwenye ukame kabla ya kuanza kufunga tena kwenye mechi dhidi ya Simba na Ihefu.
Mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe alikiri kupitia kipindi kigumu mno wakati hafungi mabao ikiwemo kuhukumiwa kwa hilo lakini alipoanza kufunga kwenye mechi ya Simba alijiona ameutua mzigo na ndiyo maana alidondosha machozi baada ya kufunga.
“Ninachoweza kusema, nimepitia kipindi kigumu sana kwenye mpira, kama msimu uliopita vingi havikwenda vizuri lakini kuna watu wengi walikuwa wakiniunga mkono, walijitahidi kuwa na mimi kuhakikisha nakuwa vizuri.
“Unajua sisi washambuliaji tunapitia vipindi tofauti hasa kama hufungi wengi watakuhukumu kwa hilo, kwa hiyo nilipofunga nikahisi nimetua mzigo, nililia kwamba labda sasa mambo yanaanza kunyooka na nashukuru nikafunga tena dhidi ya Ihefu, kikubwa nataka kuisaidia timu, napaswa kufunga ili timu isonge mbele,” alisema Dube.
Mbali ya kufunga juzi dhidi ya Ihefu na Simba, Dube pia alifunga kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi msimu huu dhidi ya Kagera Sugar, mechi ambayo walishinda kwa mabao 2-1.
Soka Mabao yamkumbusha Dube kipindi kigumu
Mabao yamkumbusha Dube kipindi kigumu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
