Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Simba umetangaza kuingia mkataba wa miaka miwili na kampuni ya bima ya MO Assurance, ambayo itakuwa ikitoa huduma ya afya kwa timu zote tatu; kikosi cha wakubwa, wanawake na vijana chini ya miaka 20 pamoja na wafanyakazi wote.
Mkataba huo wenye thamani ya Sh milioni 250, utakuwa unatoa huduma kwa mfanyakazi wa Simba pamoja na wategemezi wake wanne ili kuwafanya waongeze ufanisi kwenye majukumu yao.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema lengo kuu lilikuwa ni kuhakikisha wachezaji na wafanyakazi wote wanakuwa na bima ya afya na kwamba hilo halikuanza hivi karibuni isipokuwa ni mipango ya muda mrefu ambapo waliwashirikisha pia Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) ambao walikubaliana na mchakato huo.
“Leo tunaingia mkataba wa bima na MO Assurance, watakuwa wanatoa bima kwa wachezaji wote, benchi la ufundi na menejimenti. Lakini pia hakuna gharama yoyote kwa upande wa Simba. Kama Simba tunajivunia sana,”
“Kabla ya mkataba huu Simba ilikuwa inatumia zaidi ya Shilingi milioni 300 kwa mwaka kwa ajili ya matibabu, mkataba huu utaenda kutupunguzia gharama kwa kiasi kikubwa kwani sasa MO Assurance itakuwa inashughulikia suala hili,” alisema Barbara.
Mkurugenzi wa MO Assurance, Gregory Fortes, alisema wao kama kampuni wameamua kutoa bima ya afya kwa wachezaji na wafanyakazi wa Simba ili kuhakikisha wanatimiza majukumu yao bila ya kuwa na hofu ya maradhi.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa MeTL Group, Fatema Dewji ,alisema katika maisha ya mwanadamu afya ni muhimu sana, kwa kutambua hilo MO Assurance imekuja na habari njema kwa wachezaji wote wa Simba, benchi la ufundi, menejimenti pamoja na familia zao.
Soka Simba, Mo Assurance wasaini mkataba
Simba, Mo Assurance wasaini mkataba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
