Barcelona, Hispania
Waendesha mashitaka nchini Hispania wamemfutia kesi ya rushwa na ubadhirifu iliyokuwa ikimkabili mshambuliaji wa zamani wa Barcelona, Neymar.
Neymar ambaye kwa sasa anaichezea Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa alishitakiwa pamoja na watu wengine wakiwamo ndugu wa familia yake katika kesi inayohusu uhamisho wake kutoka klabu ya Santos ya Brazil kwenda Barcelona ya Hispania.
Uamuzi wa kumfutia kesi mshambuliaji huyo umekuja wakati awali waendesha mashitaka hao katika madai yao walitaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 afungwe jela miaka miwili pamoja na kutozwa faini ya Pauni milioni 8.6.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni wazazi wa Neymar, klabu za Barcelona na Santos, marais wa zamani wa klabu ya Barcelona Josep Maria Bartomeu na Sandro Rosell pamoja na rais wa zamani wa klabu ya Santos, Odilio Rodrigues.
Neymar ambaye alikana tuhuma zilizokuwa zikimkabili alisema kwamba hakumbuki kama alishiriki katika mazungumzo ya mkataba wake lakini makubaliano ya awali yalifikiwa mwaka 2011 kwa mchezaji huyo kuhama Santos na kujiunga na Barcelona na makubaliano hayo kukamilishwa rasmi miaka miwili baadaye.
Kampuni ya DIS ya Brazil inayojihusisha na uwekezaji ndiyo iliyolifikisha suala hilo mahakamani ikidai kuwa na umiliki wa asilimia 40 ya haki za Neymar tangu wakati mchezaji huyo akiwa na miaka 17 kwa malipo ya Euro 2 milioni, kampuni hiyo katika madai yake ilidai thamani ya mchezaji huyo ilishushwa na hivyo kukosa malipo makubwa kwani kuna klabu zilizomtaka kwa Euro 60 milioni.
Klabu ya Barcelona kwa upande wake ilidai kwamba wakati wa makubaliano ada ya Neymar ilikuwa Euro 57.1 milioni ambapo kati ya hizo Euro 40 milioni zililipwa kwa familia ya mchezaji huyo na kati ya hizo DIS ililipwa asilimia 40 ya mgao wa Euro 17.1 milioni ambazo zililipwa katika klabu ya Santos.
Mwaka 2017, Neymar ambaye pia anaichezea timu ya Taifa ya Brazil alishindwa rufaa yake katika Mahakama Kuu ya Hispania hali iliyosababisha tuhuma hizo kurudishwa mahakamani na waendesha mashitaka wa Hispania.
Awal DIS walitaka Neymar afungwe jela miaka mitano na adhabu ya kifungo jela kwa Rosell na Bartomeu na faini ya Euro 149 milioni wakati waendesha mashitaka wao walitaka adhabu ya kifungo cha miaka mitano kwa Rosell na faini ya Euro 8.4 milioni kwa klabu ya Barcelona na kifungo cha miaka miwili kwa Neymar pamoja na faini ya Euro 10 milioni pia kwa mchezaji huyo.
Kimataifa Neymar afutiwa kesi ya rushwa
Neymar afutiwa kesi ya rushwa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
