Na mwandishi wetu
Simba imeshindwa kushika usukani wa Ligi Kuu NBC, imepoteza mechi yake ya kwanza ya ligi hiyo msimu huu baada ya kuchapwa bao 1-0 na Azam katika mechi iliyopigwa Alhamisi hii usiku kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Timu ya Simba pia imetibuliwa rekodi yake ya muda mrefu ya kuinyanyasa Azam, rekodi ambayo Simba imekuwa ikijivunia kwa takriban miaka mitano sasa, katika kipindi chote hicho kwenye mechi za ligi, matokeo baina ya timu hizo yalikuwa ni sare au Azam kupoteza.
Kwa kocha Juma Mgunda ambaye tangu ajiunge na timu hiyo Septemba mwaka huu akitokea Coastal Union, naye anakuwa ametibuliwa rekodi yake ya ushindi, anakuwa amepoteza mechi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo ambayo hadi sasa anajivunia kwa kuipa heshima kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa kipigo hicho Simba sasa inashika nafasi ya tatu kwenye ligi ikibaki na pointi 14 katika mechi saba nyuma ya Mtibwa inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 15 na imecheza mechi tisa wakati Yanga wanashika usukani wakiwa na pointi 17 katika mechi saba kama za Simba.
Azam nao ushindi huo dhidi ya Simba unawafanya wapae kwenye msimamo hadi nafasi ya nne kutoka ya tisa wakiwa wamefikisha pointi 14 kama za Namungo na Singida Big ingawa Azam inabebwa na wingi wa mabao ya kufunga.
Kwenye mechi ya jana iliyojaa ufundi na ushindani wa kiwango cha juu, aliyeitibulia Simba na Mgunda rekodi za ushindi na kutopoteza mechi alikuwa ni Prince Dube aliyeifungia Azam bao katika dakika ya 35 na kuifanya Azam iwe timu ya kwanza kuifunga Simba na kubeba pointi tatu kwenye ligi msimu huu.
Simba: Aishi Manula, Nyoni, Tshabalala, Joash Onyango, Henock Inonga, Jonas Mkude/Banda, Chama, Kapanga, Kyombo/Bocco, Phiri na Okrah/Kibu.
Azam: Ahmada, Mwaikenda, Kangwa, Manyama, Amoah, Ndala, Lyanga, Akaminko, Dube/Kola, Muguna/Zayd na Kipre Jr/Nado.
Mechi zijazo za ligi ni kama ifuatavyo
Jmosi Oktoba 29, 2022
Prisons v Namungo (saa 8:00 mchana)
Geita Gold v Yanga (saa 10:00 alasiri)
Jpili Oktoba 30, 2022
Singida Big v Coastal Union
Simba v Mtibwa Sugar
