Barcelona, Hispania
Barcelona jana Jumatano imefungwa mabao 3-0 na Bayern Munich na kuaga rasmi michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) katika hatua ya makundi, huu ukiwa msimu wa pili mfululizo kwa Barca kuishia hatua hiyo.
Barca hata kama ingeifunga Bayern, bado isingeweza kufuzu kwani Inter Milan nayo imeichapa Viktoria Plzen mabao 4-1, matokeo yanayoifanya Inter kufikisha pointi 10 na Bayern yenye pointi 15 kusonga mbele katika Kundi C wakati Barca na Viktoria Plzen zikiishia hapo.
Anguko hilo la Barca linamuweka katika wakati mgumu kocha wa timu hiyo, Xavi Hernanndez ambaye msimu uliopita wakati timu yake ikicheza Europa Ligi alinukuliwa akisema kwamba hadhi ya timu hiyo si Europa Ligi, ni UCL, michuano ambayo inatajwa kuwa na hadhi kubwa, si Ulaya tu bali dunaini kote.
Xavi hata hivyo anajivunia ushindani ambao amekuwa akiuonyesha katika La Liga ingawa hapo hapo kuna wasiwasi kama ataweza kuiangusha Real Madrid katika mbio hizo na pamoja na ukweli kwamba kocha huyo anaungwa mkono na mabosi wa klabu hiyo bado hawezi kuukwepa ukweli kwamba ana kibarua kigumu.
Katika Kundi A, Napoli inaungana na Liverpool kusonga hatua ya mtoano, Napoli ikiwa kinara wa kundi hilo imefikisha pointi 15 baada ya jana kuilaza Rangers mabao 3-0 wakati Liverpool imefikisha pointi 12 na katika mechi yake ya jana kama ilivyo kwa Napoli, nayo iliilaza Ajax mabao 3-0.
Kundi B, vinara wa kundi hilo, Club Bruges wanasonga mbele wakiwa na pointi 10 wakiungana na FC Porto yenye pointi tisa wakati Kundi D hali bado tete, Tottenham inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nane bado ina kazi ya kufanya dhidi ya Sporting yenye pointi saba sawa na Frankfurt wakati Marseille inashika mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi sita.
Kocha wa Chelsea, Graham Potter ana kila sababu ya kujifariji baada ya timu yake kufuzu katika Kundi E ikiwa kinara wa kundi hilo baada ya kujikusanyia pointi 10 na kuiacha vita ngumu katika kundi hilo kwa AC Milan yenye pointi saba, RB Salzburg yenye pointi sita na Dinamo Zagreb yenye pointi nne.

Mabingwa watetezi Real Madrid wanaungana na RB Leipzig kusonga mbele katika Kundi E, Real wamefikisha pointi 10 wakati Leipzig wana pointi tisa wakati Shakhtar Donetsk na Celtic zimeaga mashindano.
Man City ikiwa kinara wa Kundi G imefuzu katika kundi hilo ikiwa na pointi 11 ikiiacha vita ya kundi hilo kwa Borussia Dortmund yenye pointi nane na Sevilla yenye pointi tano wakati FC Copenhagen imeaga katika hatua hiyo ikiwa na pointi mbili.
Matajiri wa jiji la Paris, klabu ya Paris Saint Germain (PSG) nao wamefuzu katika Kundi H wakiwa na pointi 11 na hivyo wanaingia hatua ya mtoano ambayo waliishia msimu uliopita na sasa swali linabaki, je timu hiyo itavuka hatua hiyo msimu huu. PSG imefuzu kundi hilo ikiungana na Benfica zote zikiwa na pointi 11 wakati Juventus na Maccabi Haifa zikiishia hatua ya makundi.
Timu zilizofuzu hatua ya mtoano
Bayern Munich
Inter Milan
Napoli
Liverpool
Club Bruges
FC Porto
Chelsea
Real Madrid
RB Leipzig
Man City
PSG
Benfica
Matokeo ya mechi za UCL Jumanne na Jumatano hii…
Inter Milan 4-0 Viktoria Plzen
Ajax 0-3 Liverpool
Napoli 3-0 Rangers
Atl Madrid 2-2 B Leverkusen
Barcelona 0-3 Bayern Munich
Tottenham 1-1 Sporting
Club Bruges 0-4 FC Porto
Frankfurt 2-1 Marseille
B.Dortmund 0-0 Man City
RB Salzburg 1-2 Chelsea
Celtic 1- 1 Shakhtar Donetsk
RB Leipzig 3-2 Real Madrid
PSG 7-2 Maccabi Haifa
Sevilla 3-0 FC Copenhagen
Dinamo Zagreb 0-4 AC Milan
Benfica 4- 3 Juventus
