Paris, Ufaransa
Winga wa zamani wa Bayern Munich na timu ya Taifa ya Ufaransa, Franck Ribery ametangaza rasmi kustaafu soka.
Ribery ambaye kwa sasa ana miaka 39 mbali na kutangaza uamuzi huo pia ametangaza kusitisha mkataba wake na klabu ya Serie A ya nchini Italia ya Salernitana sababu kubwa iliyochangia hatua hiyo pamoja na mambo mengine ni maumivu ya goti ambayo yamekuwa yakimuandama kwa muda mrefu.
Akiwa Bayern, Ribery ameweka rekodi ya kuifungia timu hiyo mabao 124, kutoa asisti 182 katika mechi 425 kuanzia mwaka 2007 alipojiunga na wababe hao wa Ujerumani hadi mwaka 2019 ambapo pia amebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2013 na lile la Bundesliga mara tisa.
“Mpira umesimama, fikra bado hazijasimama, asanteni wote kwa hatua hii ya kipekee,” alisema Ribery kupitia akaunti yake ya Twitter.
Ribery alijiunga na Fiorentina kabla ya kuhamia Salernitana mwaka jana majira ya kiangazi na kuisaidia klabu hiyo iliyokuwa ikipambana na kufanikiwa kujinasua na janga la kushuka daraja kwa tofauti ya pointi moja lakini hakuichezea timu hiyo tangu ilipopoteza mechi yake na AS Roma na katika siku za karibuni tayari kulikuwa na uvumi kuhusu mpango wake wa kustaafu soka.
Nyota wa Ribery ilizidi kung’ara mwaka 2007 alipojiunga na Bayern kwa ada ya Pauni 17 milioni akitokea Marseille ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuiwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Ujerumani na timu hiyo kumaliza ikiwa nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Italia.
Amewahi kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Ufaransa mara tatu, ameichezea timu ya Taifa ya Ufaransa mara 81 na kuifungia mabao 16 kabla ya kutangaza kustaafu kuichezea timu hiyo mwaka 2014 baada ya kushindwa kuiwakilisha kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huo nchini Brazil kutokana na matatizo ya mgongo.
Kimataifa Franck Ribery astaafu soka
Franck Ribery astaafu soka
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
