Manchester, England
Cristiano Ronaldo ameshutumiwa kila kona kwa kutoka uwanjani kabla ya mechi kumalizika akitakiwa aache kujiona mkubwa kuliko klabu huku kocha Erik Ten Hag akitakiwa kumuweka benchi kwa kuwa timu inacheza vizuri na kushinda bila ya yeye.
Ronaldo alitoka uwanjani kabla ya mechi kumalizika jana Jumatano usiku wakati Man United ikiumana na Tottenham na kutoka na ushindi wa mabao 2-0 huku Ronaldo akionekana kuchukizwa na kitendo cha Ten Hag kumuweka benchi bila kumpa nafasi ya kucheza.
Akizungumzia tukio hilo mshambuliaji wa zamani wa England, Gary Lineker alisema alichofanya Ronaldo kinawatoa watu katika kufurahia kiwango kizuri cha timu hiyo katika mechi dhidi ya Tottenham na ni kitu cha hovyo kisichokubalika.
Kwa upande wake nahodha wa zamani wa timu ya Wales, Ashley Williams alisema, “mechi ilikuwa nzuri kwa Man United lakini hapo hapo tunajikuta tukimzungumzia Cristiano Ronaldo ambaye hata hakucheza.
Beki wa zamani wa England, Micah Richards alisema, “kwa mmoja wa watu wenye jina kubwa kufanya jambo lile wakati timu yake inashinda ni kujiona yeye ni zaidi, inasikitisha, tabia za Ronaldo hazikubaliki na anatakiwa aruhusiwe kuondoka Januari wakati wa dirisha la usajili.
“Kocha wake alikuwa na tatizo naye mwanzo wa msimu, wakati wa maandalizi ya msimu na kitendo cha kuendelea na hilo si sawa, nafikiri kuna umuhimu wa yeye kuondoka.”
Kipa wa zamani wa Man United, Peter Schmeichel alisema Ronaldo alitakiwa kufahamu kwamba tabia zake zinamfanya avutie vyombo vya habari, “hii ni mara yangu ya kwanza kusema kwamba nimekerwa na Ronaldo, kwa kawaida huwa namuunga mkono, naielewa hali yake.”
“Tuko katika kipindi cha mpito, Manchester United hadi sasa imekuwa chini ya makocha watano tangu Sir Alex Ferguson aondoke. Tumempata Erik ten Hag ambaye ana mawazo yaliyo wazi kuhusu namna anavyotaka timu icheze soka, tunahitaji kuelewana na kila mtu kumpa mwenzake muda, hatutaki mifarakano kama hii, inakera,” alisisitiza Schmeichel.

Naye Mike Greenwood alisema kwamba Ronaldo anajitenga na kikosi cha sasa, wakati wote alitakiwa abaki kuwa mkongwe wa Old Trafford lakini kwa sasa anahitaji kuwekwa kando kwenye kikosi kwa sababu anafanya mabaya kuliko mazuri.
Gabby Agbonlahor alimtaja Ronaldo kuwa ni wa hovyo na mharibifu akimtaka Ten Hag kumuweka benchi katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Chelsea.
“Ana miaka 37 na amekuwa na maisha mazuri ya soka na huenda ni mmoja wa wachezaji bora wa soka, timu yake inacheza vizuri na imeichapa Tottenham, Man United inacheza vizuri bila ya kuwa na Ronaldo, alicheza vizuri akitokea benchi katika mechi dhidi ya Everton na kufunga goli lakini alipoanza katika mechi na Newcastle hakucheza vizuri hadi akatolewa,” alisema Agbnolahor.
“Namuunga mkono Ten Hag kwa kutokuwa na presha ya kumpanga Ronaldo, kutoka uwanjani kabla ya mechi na kwenda nyumbani, kwangu ni jambo la hovyo,” alisema.
Agbonlahor pia alikiri kwamba Ronaldo ni mchezaji mzuri mwenye rekodi ya kufunga mabao 700 lakini hawezi kuwakosea heshima wachezaji wenzake kwa kujiona yeye ndio yeye.
Mtu pekee aliyeshindwa kumshutumu Ronaldo ni beki wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand ambaye alisema kwamba alidhani kitendo cha mchezaji huyo kuwekwa benchi ni kwa sababu ya kumuandaa kwa mechi ijayo dhidi ya Chelsea na kwamba jambo hilo ndilo lililomkera Ronaldo.
Ferdinand alimgeuzia kibao Ten Hag akimtaka kuwa makini kwenye usajili ujao na kufikiria vizuri kile anachokifanya. “Kama anaona Ronaldo hafai kuanza kipindi cha kwanza kwenye timu yake mara kwa mara, nafikiri anatakiwa aachane naye, amruhusu aondoke.”
Hii si mara ya kwanza kwa Ronaldo kudhihirisha hasira zake waziwazi na kutoka uwanjani kabla ya mechi kumalizika, alifanya hivyo katika mechi ya maandalizi ya msimu wa 2022-23 dhidi ya Rayo Valecano alipotoka uwanjani kwa hasira na kuondoka na Jumapili iliyopita alionyesha hasira zake waziwazi baada ya Ten Hag kumtoa katika mechi dhidi ya Newcastle.
