Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imekiri kupewa mpinzani mgumu, Club Africain ya Tunisia kwenye mechi ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini imeahidi kupambana kuhakikisha inauvuka mtihani huo na kutinga hatua ya makundi.
Yanga imepangwa kucheza na Africain baada ya kukubali kipigo cha jumla cha mabao 2-1 kutoka kwa Al Hilal ya Sudan kwenye hatua ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kwao ni changamoto ngumu waliyokutana nayo na hiyo inatokana na michuano wanayoshiriki ambayo hujumuisha timu bora kutoka nchi tofauti, hivyo lazima kuwe na ugumu.
Alisema wapinzani wao ni timu kongwe na kubwa Tunisia na wamekuwa wakifanya vizuri pia kwenye michuano hiyo, hivyo wanatambua nini wanapaswa kukifanya na watakuwa na maandalizi makubwa kwa ajili ya timu hiyo.
“Ni droo ngumu, ni timu ngumu maana aidha upo Ligi ya Mabingwa Afrika au Shirikisho ni lazima ukutane na timu ambazo zinafanya vizuri kwenye ligi zinakotoka, Africain wote wanafahamu ni timu kubwa pale Tunisia nyuma ya Esperance wanafuatia wao kwa kutwaa mataji mengi.
“Lakini pia tunafahamu timu za Tunisia zina rekodi nzuri kwenye hii michuano ukiondoa timu za Morocco, kwa hiyo tunatambua ugumu ambao tumeupata baada ya droo hii lakini tunatambua tupo kwenye michuano hii kwa ajili ya kushindana na timu kubwa kwa hiyo tumeipokea vizuri na tupo tayari kwa changamoto nzuri na kuhakikisha timu inacheza makundi pia kwenye shirikisho,” alisema Kamwe.
Africain itakuwa inarejea mara ya pili Tanzania kwenye michuano hiyo msimu huu baada ya hatua iliyopita kuumana na Kipanga FC ya Zanzibar ambapo matokeo ya jumla Kipanga ilibamizwa mabao 7-0 na kuaga michuano hiyo.
Yanga itakuwa mwenyeji kwenye mechi ya awali dhidi ya Watunisia hao ambayo itapigwa Novemba 2 kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Novemba 9, mwaka huu nchini Tunisia.
Soka Yanga yakiri Africain wagumu
Yanga yakiri Africain wagumu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
