Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry amemshutumu mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe baada ya kuwapo habari za mshambuliaji huyo kutaka kuhama PSG akidai hafurahii kupangwa mshambuliaji pekee hapo hapo akidai kudanganywa na mabosi wa klabu hiyo.
Mbappe ambaye majira ya kiangazi mwaka huu alisaini mkataba na PSG unaofikia ukomo mwaka 2025 baada ya PSG kuizidi ujanja Real Madrid iliyokuwa ikimuwania mshambuliaji huyo, sasa anataka kuwahama vigogo hao wa Ufaransa Januari mwakani ingawa PSG imekana kuwapo madai ya mchezaji huyo kutaka kuhama.
Mbappe amekuwa akipangwa mshambuliaji pekee wa kati huku Lionel Messi na Neymar wakicheza pande nyingine mbili wakati akiwa Ufaransa anakuwa huru zaidi ambapo mara nyingi amekuwa akicheza na Giroud.
“Hakuna anayependa udhaifu wake uwekwe hadharani, ni kawaida hilo hakuna anayelitaka, lakini kuna kitu ambacho ni kikubwa kuliko vingine vyote, na hicho ni klabu,” alisema Henry ambaye mbali na Arsenal pia aliwahi kutamba na Barcelona.
“Lakini je walimfanya aone kama klabu ni kitu muhimu au walimfanya ajione yeye ni muhimu kuliko klabu?” alihoji Henry ambaye pia alikuwa mfungaji bora wa timu ya Taifa ya Ufaransa na kuongeza kuwa hata yeye wakati akiwa Barcelona alikumbana na hali kama hiyo.
“Nitaitumia stori yangu mwenyewe, sikuwa nikipenda kucheza mbele zaidi na pembeni wakati nikiwa Barcelona lakini nilicheza kwa sababu ya timu,” alisema Henry.
“Sikupenda nikiwa tayari nimecheza mechi 100 za timu ya Taifa na sijui mabao mangapi niliifungia Ufaransa huko nilitakiwa kucheza upande wa kushoto, sikuwahi kumsikia yeyote akisema kwa mshangao ooh ni jambo zuri anacheza upande wa kushoto badala ya wachezaji wenye mechi chache za timu ya Taifa na mabao machache,” aliongeza Henry.
“Kuna kanuni moja tu, kama bosi akikutaka ufanye jambo, unatakiwa kulifanya kama ni zuri kwa ajili ya timu na kama ni baya hapo nitaingia katika mjadala,” alisema.
Kimataifa Thierry Henry amtolea uvivu Mbappe
Thierry Henry amtolea uvivu Mbappe
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
