Madrid, Hispania
Klabu ya Atletico Madrid hatimaye imemsajili kwa mara nyingine mshambuliaji Mfaransa, Antoine Griezmann kutoa Barcelona kwa mkataba wa kudumu utakaofikia ukomo mwaka 2026.
Mwaka 2019, Griezmann alikuwa miongoni mwa wachezaji ghali akijiunga na Barcelona kwa ada ya Pauni 108 milioni akitokea Atletico, aliifungia timu hiyo jumla ya mabao 35 katika mechi 102 kabla ya kurudi kwa mara nyingine Atletico msimu uliopita kwa mkopo wa miaka miwili.
Kwa msimu huu, Griezmann mwenye umri wa miaka 31 ana mabao matatu hadi sasa katika mechi 11 ingawa kati ya mechi hizo ni tatu tu ambazo ameanzia kipindi cha kwanza, nyingine zote amekuwa akitokea benchi na mara nyingi amekuwa akicheza dakika zisizozidi 30.
Kwa mujibu wa mchambuzi mmoja uamuzi wa Griezmann kucheza kwa dakika 30 kila mechi umetokana na kuwapo kwa kipengele katika mkataba wa mkopo wa mchezaji huyo kinachoitaka Atletico kumnunua kwa Euro 40 milioni kama atacheza kwa zaidi ya dakika 45 katika asilimia 50 ya mechi za msimu za Atletico.
Katika kukabiliana na hali hiyo kocha wa Atletico, Diego Simeone amekuwa akimpanga Griezmann kuingia kipindi cha pili kila baada ya dakika 60 za mchezo katika mechi nane kati ya 11 msimu huu ili kuhakikisha kipengele hicho hakiibani klabu hiyo.
Baada ya kumpa mkataba wa kudumu huenda Atletico sasa ikaanza kumtumia kuanzia kipindi cha kwanza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayochezwa keshokutwa Jumatano dhidi ya Club Brugge.
Kimataifa Atletico yambeba jumla Griezmann
Atletico yambeba jumla Griezmann
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
