London, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amekiri timu yake haimo katika ushindani wa taji la Ligi Kuu England (EPL) baada ya kipigo cha mabao 3-2 mbele ya Arsenal na kujikuta wakiwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 14.
Liverpool imecheza mechi nane hadi sasa, imeshinda mbili tu kati ya hizo wakati vinara wa ligi hiyo Arsenal wana pointi 24 na wamecheza mechi tisa rekodi ambayo imetosha kumfanya Klopp akate tamaa kwenye mbio za kuliwania taji hilo kwa sasa. “Hatumo kwenye mbio za ubingwa,” alisema Klopp.
Klopp hata hivyo pamoja na hali hiyo pia alizungumzia namna timu yake ilivyoisumba Arsenal, “kwa hiyo tuna matatizo kwa wakati huu lakini tuliwasumbua wapinzani wetu, vinara wa ligi tuliwapa shida nyingi japo kwa upande wetu tuko katika hali mbaya, kwa mabadiliko ya mapema, tuliwasababishia matatizo, huo ndio ukweli na tunatakiwa kuendelea hivyo,” alisema.
“Ni kweli kwamba pamoja na hali tuliyonayo tumecheza na Arsenal, tunacheza na Rangers na baadaye tunacheza na Man City, je hao ni wapinzani sahihi wa kurudisha hali ya sisi kujiamini, nadhani siyo lakini tutakwenda kupambana, hicho ndicho tunacholazimika kukifanya na ndicho tunachokifanya,” alisema Klopp.
“Tuko katika kipindi kigumu na tunataka kukipita kipindi hiki pamoja na hilo ndilo tunalolifanyia kazi kwa sasa,” aliongeza Klopp.
Klopp pia aliizungumzia penalti waliyopewa Arsenal ambayo ilitolewa baada ya Thiago Alcantara kumchezea rafu Gabriel Jesus na kuipatia Arsenal bao la ushindi lililofungwa na Saka ingawa mazingira ya rafu yalionekana kujaa utata na Liverpool kuona kama refa aliwaonea kwa kuipa Arsenal penalti.
“Nini ninachoweza kusema katika mazingira haya? Alifikiria haraka haraka ikawa penalti jambo ambalo linafurahisha lakini huo ni uamuzi wake na mwingine akaangalia na akafikiria hivyo hivyo kwamba ni penalti, na tunajua katika maisha, kama marefa wawili wakiwa na mtazamo mmoja huo unakuwa ndio ukweli kwa hiyo tunatakiwa kuishi katika hali hiyo,” alisema.
“Lakini nikirudia kuangalia tena na kutafakari kama kulikuwa na hali ya kugusana sina hakika kama kulikuwa na jambo hilo na kama lilikuwapo basi ni kwa kiwango kidogo tu lakini mchezaji alianza kwenda chini, akaenda tena na miguu yote hadi chini, hiyo ni ishara kwamba kuna kitu kilikuwa kikitengenezwa lakini kwa refa hilo halikuonekana,” alisema Klopp.
Kimataifa Klopp aanza kukata tamaa
Klopp aanza kukata tamaa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
