London, England
Arsenal imeendeleza kasi yake ya ushindi katika Ligi Kuu England (EPL) baada ya kuichapa Liverpool mabao 3-2 na kuiengua Manchester City kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Ushindi huo wa Jumapili hii unaifanya timu kufikisha pointi 24 dhidi ya 23 za Man City ambayo ushindi wao wa Jumamosi wa mabao 4-0 dhidi ya Southampton uliwafanya washike usukani kwa takriban saa 24, timu zote hadi sasa zimecheza mechi tisa.
Alikuwa ni Gabriel Martinelli aliyeipatia Arsenal bao la mapema katika dakika ya kwanza tu ya mchezo huo akiitumia pasi ya Odegaard lakini Liverpool walikuja juu na kusawazisha bao hilo dakika ya 34 kupitia kwa Darwin Nunez ambaye aliitumia krosi ya Luis Diaz kufunga bao hilo.
Dakika chache kabla ya timu kwenda mapumziko, Arsenal walipata bao la pili lililofungwa na Bukayo Saka akiitumia pasi ya Martinelli na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Arsenal ikiwa mbele.
Dakika nane baada ya kuanza kipindi cha pili, Liverpool walifanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Roberto Firmino aliyeinasa pasi ya Jota lakini dakika ya 76, mkwaju wa penalti uliopigwa na Saka ulitosha kuipatia Arsenal bao la tatu na la ushindi. Penalti hiyo ilitolewa baada ya Thiago Alcantara kumchezea rafu Gabriel Jesus.
Katika mechi nyingine ya Jumapili, Cristiano Ronaldo alifunga bao la ushindi na kuiwezesha Man United kutoka uwajani na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Everton.
Wenyeji Everton ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya tano lililofungwa na Iwobi lakini Dos Santos aliisawazishia Man United katika dakika ya 15 akiitumia pasi ya Antony Martial kabla Ronaldo hajaandika bao la pili dakika moja kabla ya mapumziko akiitumia pasi ya Casemiro. Kwa Ronaldo bao hilo linakuwa na maana kubwa kwani anakuwa ameweka rekodi ya kufikisha mabao 700.
Matokeo ya mechi za wikiendi EPL…
Crystal Palace 2-1 Leeds
West Ham 3-1 Fulham
Arsenal 3-2 Liverpool
Bournemouth 2-1 Leicester
Chelsea 3-0 Wolves
Man City 4-0 Southampton
Newcastle 5-1 Brentford
Brighton 0-1 Tottenham
Everton 1-2 Man United
Kimataifa Arsenal yaipiga Liverpool, yashika usukani
Arsenal yaipiga Liverpool, yashika usukani
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
