New York, Marekani
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka tisa, mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe ameongoza orodha ya wanasoka wanaolipwa fedha nyingi akiwabwaga vinara wa mara kwa mara wa orodha hiyo, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo huku mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland akiingia 10 bora.
Taarifa za Jarida la Forbes zilizopatikana Ijumaa hii zilieleza kuwa Mbappe ambaye ndio kwanza ana umri wa miaka 23 kwa msimu huu atavuna kiasi cha Dola 128 milioni ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 290.
Anayeshika nafasi ya pili katika orodha hiyo ni mshambuliaji mwingine wa PSG, Messi ambaye kwa mujibu wa Forbes pato lake litafikia Dola 120 milioni kwa msimu huu wakati Ronaldo anayeichezea Manchester United kwa sasa anashika nafasi ya tatu pato lake likifikia Dola 100 milioni.
Nafasi ya nne inashikwa na mshambuliaji mwingine wa PSG, Neymar ambaye pato lake linafikia Dola 87 milioni akifuatiwa na mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah ambaye pato lake linafikia dola 53 milioni.
Kwa muda mrefu orodha hiyo ya Forbes imekuwa ikitawaliwa na Ronaldo na Messi, mara ya mwisho mchezaji pekee aliyeweza kuwabwaga mastaa hao ni nahodha wa zamani wa England, David Beckham na hiyo ilikuwa mwaka 2013.
Pato la Mbappe kwa kiasi kikubwa limechangiwa na mkataba mnono wa miaka mitatu aliosaini na klabu hiyo ya Ufaransa mwezi Mei mwaka huu, usajili ambao ulifuta uvumi wa muda mrefu uliomhusisha na mipango ya kusajiliwa na klabu ya Real Madrid ya Hispania.
Mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland ambaye tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani amekuwa tishio kwa upachikaji mabao, naye yumo kwenye 10 bora ya orodha hiyo akiwa nafasi ya sita ambapo pato lake linafikia Dola 39 milioni wakati mshambuliaji wa Barcelona Robert Lewandowski ni wa saba, pato lake likifikia Dola 35 milioni.
Orodha ya 10 bora inakamilishwa na Eden Hazard wa Real Madrid (Dola 31 milioni), Andre Iniesta wa Vissel Kobe (Dola 30 milioni) na Kevin de Bruyne wa Man City (Dola 29 milioni).
Kimataifa Mbappe awapiku Messi, Ronaldo kwa mkwanja
Mbappe awapiku Messi, Ronaldo kwa mkwanja
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
