Paris, Ufaransa
Lionell Messi ambaye anajiandaa kucheza fainali zake za tano za Kombe la Dunia akiwa na timu ya Argentina, ni kama vile ameanza kuaga bada ya kusema kwamba hizo zitakuwa fainali zake za mwisho za michuano hiyo.
Messi mwenye umri wa miaka 35 sasa hata hivyo kauli yake hiyo bado imeacha swali kwamba baada ya fainali hizo atastaafu kuichezea timu hiyo au ataendelea na badala yake hatokuwapo katika fainali nyingine za Kombe la Dunia za mwaka 2026.
Fainali za Kombe la Dunia za Qatar zitaanza kutimua vumbi Novemba 20 mwaka huu na Messi amesema kwamba ana shauku kubwa ya kushiriki kwenye fainali hizo ambazo amesisitiza kwamba ni za mwisho kwake. “Kuna hali ya wasiwasi na hamasa wakati huo huo, hizi ni fainali za mwisho kwangu,” alisema Messi ambaye pia mchezaji wa klabu ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Messi kuzungumzia mambo yake yajayo baada ya michuano hiyo na hapana shaka kwamba ana shauku ya kulibeba taji hilo kwa mara yake ya kwanza akiwa na Argentina, timu yenye matumaini makubwa yanayotokana na rekodi nzuri ya mechi 35 zilizopita bila kupoteza hata mchezo mmoja.
Mafanikio makubwa ya kukumbukwa hivi karibuni kwa Argentina ni pale walipolibeba taji la Copa America mwaka jana wakiwabwaga wenyeji Brazil, jambo ambalo Messi anaamini kuwa ni hatua nzuri ya kuelekea kwenye mafanikio.
“Katika Kombe la Dunia lolote linaweza kutokea, mechi zote ni ngumu mno, timu zinazopewa nafasi ya kushinda si lazima zishinde, sijui kama na sisi ni timu inayopewa nafasi hiyo au la lakini wakati wote Argentina ni timu iliyo kwenye nafasi hizo kwa sababu ya historia yetu na kwa sasa hilo ni zaidi lakini sidhani kama tunapewa nafasi kubwa zaidi kwa kuwa zipo timu zilizo juu yetu” alisema Messi.
Argentina ilibeba Kombe la Dunia mwaka 1978 na 1986 na katika fainali za Qatar imepangwa Kundi C ambalo pia lina timu za Poland, Mexico na Saudi Arabia na itaanza kurusha karata yake Novemba 22 dhidi ya Saudi Arabia.
“Kimwili najioni niko fiti, nilikuwa vizuri kuanzia wakati wa maandalizi ya msimu mwaka huu jambo ambalo halikuwezekana mwaka uliopita (nilipohama kutoka Barcelona kuja PSG), hilo limekuwa kitu muhimu kilichoniwezesha kuuanza msimu vizuri, nimeanza msimu nikiwa mwenye shauku ya kipekee na kiakili niko vizuri,” alisema Messi.
Kimataifa Messi aanza kuaga Argentina
Messi aanza kuaga Argentina
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
