Jakarta, Indonesia
Mkuu wa Polisi Jimbo la Malang, Indonesia na polisi tisa wameondolewa katika nafasi zao na wengine 18 wakichunguzwa kutokana na vifo vya mashabiki 125 vilivyotokana na vurugu zilizotokea kwenye mechi ya soka.
Awali taarifa zilieleza kuwa mashabiki waliofariki ni zaidi ya 170 lakini taarifa za baadaye zilieleza kuwa idadi kamili ya mashabiki waliofariki baada ya polisi kufyatua mabomu ya machozi ni 125 wakiwamo watoto 17.
Tukio hilo ambalo lilitokea Jumamosi usiku mara baada ya mechi ya mahasimu wa soka nchini Indonesia timu za Arema FC na Persebaya Surabaya kumalizika huku Surabaya ikiwa mbele kwa mabao 3-2 ndipo mashabiki wa timu mwenyeji ya Arema walipovamia uwanja hali iliyowafanya polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.
Awali ilielezwa kuwa waandaaji wa mechi hiyo walipiga marufuku mashabiki wa timu iliyokuwa ugenini ya Surabaya kuingia uwanjani kwa sababu ya historia ya matukio ya vurugu za kwenye soka nchini humo hasa katika mechi zilizozoeleka kwa muda mrefu kuwa ni za timu mahasimu.
Akizungumzia tukio hilo, kocha wa Arema, Javier Roca aliwaomba msamaha wanafamilia waliopoteza ndugu zao pamoja na wale ambao wapo kwenye matibabu mahospitalini.
Jumatatu usiku mashabiki wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 1000 wakiwa na mavazi yenye rangi nyeusi waliandamana kwa amani katika mitaa mbalimbali ya jiji la Jakarta huku wakifanya maombi maalum kwa mashabiki waliopoteza maisha katika janga hilo.

Mashuhuda wa tukio hilo walidai kwamba mashabiki wanaodaiwa kufikia 42,000 wengi wao walivamia uwanjani wakionyesha hasira baada ya timu yao kufungwa mabao 3-2 hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kupoteza mechi kwenye uwanja wao wa nyumbani katika kipindi cha miaka 23.
Baadhi ya mashabiki hao walionekana wakirusha chupa na silaha nyinginezo kwa maofisa wa soka ikiwamo kuchoma moto magari ya polisi ambapo inadaiwa kwamba magari matano ya polisi yaliyokuwa uwanjani hapo yalichomwa moto na mengine kupinduliwa.
Habari zaidi zilidai kwamba vifo vingi vilitokea baada ya polisi waliojaribu kuwatuliza mashabiki hao kuanza kutumia mabomu ya machozi hadi majukwaani hali ambayo ilizua taharuki kwa mashabiki hao walioanza kuhangaika wakitafuta mahali pa kutokea.
Mbali na watoto 17 waliofariki, watoto wengine saba wanaendelea na matibabu huku polisi wapatao 323 wakiwa wamejurihiwa baadhi yao hadi sasa hali zao ni mbaya.
Uchunguzi wa polisi ambao utahusisha kamera zilizokuwa uwanjani hapo, picha za video za kwenye simu za waathirika wa tukio hilo pamoja na vyanzo mbalimbali ili kubaini chanzo hasa cha tatizo pamoja na kuwabaini watu ambao wamelitumia tukio hilo kufanya uharibifu na wizi wa mali.
