Manchester, England
Manchester Derby imekuwa tamu kwa Erling Haaland, si tu ameitumia kuendeleza rekodi ya mabao, bali pia ameitumia kuweka rekodi mpya wakati Man City ikiichapa Man United mabao 6-3.
Katika mechi ya timu hizo mahasimu iliyopigwa Jumapili hii Etihad, mabao yote ya City yalifungwa na wachezaji wawili tu, Haaland na Phil Foden, wote wamepiga hat trick huku kwa Haaland hiyo ikiwa ni rekodi ya kupiga hat trick ya tatu katika Ligi Kuu England akiwa uwanja wa nyumbani lakini pia anazidi kuwa tishio kwa kuzifumania nyavu akiwa ndiye anayeongoza katika ligi hadi sasa kwa mabao yake 14.
Foden ndiye aliyefungua karamu hiyo ya mabao katika dakika ya nane kabla Haaland hajaongeza mawili dakika za 34 na 37 na Foden kumalizia bao la nne dakika ya 44 na kuifanya City iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.
Kipindi cha pili, Haaland akaongeza bao dakika ya 64 na kukamilisha hat trick yake wakati hat trick ya Foden ilikamilika dakika ya 72. Man United nao walipambana na kupata mabao yao matatu katika dakika za 56 mfungaji akiwa Dos Santos na Martial aliyefunga mabao mawili katika dakika za 84 na la mwisho akilifunga kwa penalti katika dakika za nyongeza.
Kasi ya Haaland imekuwa ikishangaza wengi na mmoja wao ni kipa wa zamani wa Man United na Man City, Peter Schmeichel ambaye alinukuliwa na Radio BBC akisema, “Unaona wachezaji tofauti kwa Haaland, ni kama vile washambuliaji bora katika mmoja.”
“Jambo kubwa kwa mshambuliaji mzuri ni utulivu, nimecheza dhidi ya washambuliaji bora na pale wanapokosa nafasi ndipo wewe unapojikuta ukiwa makini, kina Cristiano Ronaldo, kina Filippo Inzaghi wa dunia hii wameondoka na ghafla nafasi yao imepata mtu.”
“Unapomuangalia Haaland unawaona wachezaji tofauti, ni kama vile Zlatan (Ibrahimovic) anavyofunga na hapo hapo ni kama Ronaldo, unawaona washambuliaji walio bora kwa mshambuliaji mmoja.”
“Na ndio maana anakuwa hatari, ana ile raha ya kuwaona washambuliaji wengi wa kiwango cha juu na wote wanachanganywa na kuwa mchezaji mmoja.
Haaland mwenyewe alipoulizwa kuhusu alivyoyaona matokeo hayo alisema, “naam, si mabaya, tumefunga mabao sita, nini kingine ninachoweza kusema, kushinda nyumbani, kufunga mabao sita ni jambo zuri, mwisho wa yote ni ushindi wa kipekee, hakuna cha kusema zaidi ya hilo.”
“Sijawahi hapo kabla kufunga hat-trick tatu katika mechi tatu za nyumbani, hili ni jambo la kipekee, kujiamini wakati wote limekuwa jambo zuri, baada ya kufungwa na Liverpool kwenye Ngao ya Jamii bado haikuwa jambo baya, ni jambo zuri kwamba hii mechi imekuja na nilijua kwamba natakiwa kuwa tayari,” alisema.
“Siku chache kabla ya hii Manchester Derby nilijiaminisha kwamba kuna kitu cha kipekee kitatokea na mambo mazuri ya kipekee yametokea, ni jambo zuri, hizi ni aina ya mechi ninazotaka kucheza.” alisema.
Kwa upande wake kocha wa Man City, Pep Guardiola alisema kwamba takwimu za za mabao za Haaland zinatisha, “namba zinamzungumza yeye, amewahi kufanya hivyo hapo kabla, si tu kwamba imekuwa hivyo ila wakati wote tunajaribu kumsaidia katika mazingira yetu, tuna ule mtazamo mzuri kwamba wakati wote anaonekana mwenye njaa ya mabao, na ni mshindani, namba zake zinatisha.
Kwa mabao 14 ambayo Haaland ameyafunga hadi sasa katika Ligi Kuu England, anafuatiwa kwa mbali na Harry Kane wa Tottenham mwenye mabao saba, na kwa namna namba zake za mabao zinavyoongezeka na kuwa tishio haitokuwa ajabu mwisho wa msimu akiwa mfungaji bora.
Kimataifa Haaland aweka rekodi, namba zake tishio
Haaland aweka rekodi, namba zake tishio
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
