Malang, Indonesia
Mashabiki wapatao 170 wanadaiwa kufa na wengine 180 kujeruhiwa Jumamosi usiku nchini Indonesia baada ya vurugu kutokea kwenye mechi ya mahasimu wa soka nchini humo timu za Arema FC na Persebaya Surabaya.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi wa Jimbo la Java Mashariki, chanzo cha vurugu hizo zilizotokea kwenye Uwanja wa Kanjuruhan baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa, inadaiwa kuwa ni mashabiki wa timu ya Arema kuvamia uwanja sababu ikiwa ni kutoridhishwa na matokeo ya timu yao kufungwa mabao 3-2 na mahasimu wao Surabaya.
Polisi waliokuwa uwanjani hapo baada ya kuona hali inakuwa mbaya walijaribu kuwazuia mashabiki hao kwa kutumia mabomu ya machozi hali iliyosababisha mashabiki kuanza kukimbia wakiwakwepa polisi na hivyo kuwa chanzo cha vifo na majeruhi.
Kutokana na vurugu hizo baadhi ya mashabiki inadaiwa walikosa pumzi na wengine kukanyagana hadi kufa huku habari zaidi zikidai kwamba kati ya waliokufa katika tukio hilo wamo polisi wawili.
Tayari tukio hilo limetajwa kuwa ni miongoni mwa majanga makubwa yaliyosababisha vifo kwenye soka huku taarifa ya Serikali nchini Indonesia ikiagiza kusimamishwa kwa mechi zote za soka nchini humo ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kufanyika kujua chanzo cha tukio hilo.
Katika hatua nyingine, Fifa inadaiwa kutoa taarifa ya kutounga mkono matumizi ya mabomu ya machozi kama njia mojawapo ya kutawanya mashabiki pindi zinapotokea vurugu kwenye mechi za soka.
Vurugu katika mechi za soka nchini Indonesia si jambo geni hasa katika mechi za mahasimu wa siku nyingi nchini humo, timu za Arema FC na Surabaya kiasi kwamba baadhi ya mashabiki walipigwa marufuku kununua tiketi za mechi hiyo kwa hofu ya kutokea vurugu.
Taarifa nyingine ya Serikali iliyopatikana kwenye mtandao wa Instagram ilieleza kuwa jumla ya tiketi 42,000 ziliuzwa kwa ajili ya mechi hiyo wakati Uwanja wa Kanjuruhan una uwezo wa kuchukua mashabiki 38,000 tu.
Moja ya tukio kubwa la vifo kwenye viwanja vya soka ni lile lililowahi kutokea nchini Peru mwaka 1964 baada ya mashabiki 320 kufariki na wengine zaidi ya 1,000 kujeruhiwa katika mechi ya awali ya kufuzu Michezo ya Olimpiki kati ya Argentina na Peru.
Kimataifa Mashabiki 170 wafariki Indonesia
Mashabiki 170 wafariki Indonesia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
