Manchester, England
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ametoa angalizo kabla ya kuivaa Manchester United akisema kwamba timu yake inatakiwa iwe kamili kama ina nia ya kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England.
Timu hizo mahasimu wa jiji la Manchester zinaumana leo katika mechi maarufu ya Manchester Derby huku Man Utd wakiwa na rekodi ya kupoteza mechi mbili tu kati ya nane ilizokuwa ugenini Etihad ikiwa imeshinda tatu kati ya nne za mwisho, rekodi ambayo Pep anaiona kuwa ni tishio kwake.
“Ni lazima tucheze soka sahihi Jumapili, wanaweza kukuadhibu katika sehemu ndogo tu, hatuwezi kuwa wazembe, unachotakiwa ni kuwa mpambanaji, lazima upange cha kufanya kabla ya kukifanya, kutulia na kuchukua maamuzi sahihi, unapokuwa kama uliyevurugwa ni vigumu kuchukua maamuzi sahihi,” alisema Pep.
“Wakati wote huwa natarajia ubora kutoka kwa wapinzani wetu, kiwango walichonacho kwa miaka mingi si cha kutilia shaka. Utakuwa mpambano mkubwa katika jiji, na najaribu kufikiria nini ambacho watakifanya na nini ambacho sisi tunaweza kukifanya ili kuwafunga, naisubiria mechi,” alisema Pep.
“Watu wanapofurika uwanjani wanatuweka katika hali ya presha lakini hilo ni muhimu, napenda wawe wachangamfu, wajae hamasa na kutaka kilicho bora kutoka kwetu. Unapokuwa juu unapata wapinzani zaidi, ukiwa katikati wapinzani wanapungua, ushindani mkubwa unakufanya uwe bora,” aliongeza Pep.
Man Utd baada ya kuanza msimu vibaya kwa kupoteza mechi mbili, hatimaye ilibadilika na hadi sasa inashika nafasi ya tano ikiwa imeshinda mechi nne mfululizo, mafanikio ambayo pia yamemuwezesha kocha Erik ten Hag kutwaa tuzo ya kocha bora wa mwezi Septemba na bila shaka mafanikio hayo ndiyo yanayomfanya Pep kuwataka wachezaji wake waingie uwanjani wakiwa kamili ili kupata ushindi.
Kwa upande wa Man City, bila shaka itaingia uwanjani ikiwa na dhamira ya kutopoteza hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi ikiwa tayari imeshinda mechi tano kati ya saba na kutoka sare mbili na kilichobaki ni dakika 90 za leo kuamua kama rekodi hiyo itavurugwa na Man Utd au la.
Man City katika mechi ya leo itamkosa beki John Stones aliyeumia wakati akiiwakilisha England dhidi ya Ujerumani katika mechi ya Uefa Nations Ligi pamoja na Kalvin Phillips ambaye anasumbuliwa na maumivu ya bega.
Kimataifa Pep atoa angalizo kabla ya kuivaa Man Utd
Pep atoa angalizo kabla ya kuivaa Man Utd
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
