Manchester, England
Kama unafikiria Cristiano Ronaldo atastaafu soka la kimataifa mwaka huu baada ya fainali za Kombe la Dunia, sahau, mchezaji huyo kwa sasa anazifikiria fainali za Ulaya 2024 (Euro 2024).
Ronaldo ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa ya Ureno, alitoa kauli hiyo Jumanne jioni katika hafla iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Ureno (FPF) ambapo alipewa tuzo ya kuwa mfungaji mwenye mabao mengi kwenye timu ya Taifa.
Kwa sasa mchezaji huyo wa Man United ana miaka 37, umri ambao katika hali ya kawaida angekuwa amestaafu soka la ushindani lakini anaonekana kuwa fiti na kama atapata nafasi ya kucheza fainali za Euro 2024 atakuwa amefikisha umri wa miaka 39.
Pamoja na umri kwenda lakini Ronaldo bado anaonekana kuwa na uwezo kiasi kwamba klabu yake ya Man United haikuwa tayari kumruhusu aondoke katika kipindi cha usajili cha majira ya kiangazi kwa alichodai kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag kwamba mchezaji huyo yupo katika hesabu zake.
Akizungumzia mipango yake ya Euro 2024, Ronaldo alisema, “safari haijafika mwisho, ninajivunia kupewa tuzo ya aina hii, nime-miss kupewa tuzo na sikuwahi kuwaza kwamba kuna siku nitapata mafanikio haya, namshukuru kila mmoja ambaye amekuwa muhimu katika maisha yangu ya soka, ni safari ndefu lakini ningependa kusema kwamba safari hii haijafika mwisho, jiandaeni kwa mengine kutoka kwa Cris (Ronaldo).
Tangu aanze kuichezea timu ya Taifa ya Ureno mwaka 2003, Ronaldo amefunga mabao 117 katika mechi 189 akiwa amevunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Ali Daei wa Iran kwenye timu za Taifa.
“Bado najiona niliyejaa hamasa, matamanio yangu yako juu, nipo katika timu yenye vijana, nataka niwe kwenye Kombe la Dunia na fainali za Ulaya, nafikiria hivyo,” alisema Ronaldo ambaye pia ana tuzo tano za Ballon d’Or na ndiye nahodha aliyeiongoza Ureno kutwaa taji la Euro 2016.
Kimataifa Ronaldo apiga hesabu za Euro 2024
Ronaldo apiga hesabu za Euro 2024
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
