London, England
Kinda wa Arsenal mwenye umri wa miaka 15, Ethan Nwaneri Jumapili aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza Ligi Kuu England (EPL) akiingia dakika za nyongeza wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Brentford.
Nwaneri aliingia kuchukua nafasi ya Fabio Vieira wakati Arsenal iliyokuwa ugenini tayari ikiwa na mabao hayo yaliyofungwa na Vieira, William Saliba na Gabriel Jesus na kuipa timu hiyo ushindi ambao umeiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Wakati anacheza mechi hiyo, Nwaneri alikuwa na miaka 15, miezi mitano na siku 23 na hivyo amevunja rekodi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Harvey Elliot wa Liverpool aliyeanza kucheza katika ligi hiyo akiwa na miaka 16 na siku 30 wakati kwa upande wa Arsenal anakuwa amevunja rekodi ya Cesc Fabregas ambaye alicheza kwa mara ya kwanza katika ligi hiyo akiiwakilisha Arsenal akiwa na miaka 16, miezi mitano na siku 24.
Akimzungumzia mchezaji huyo kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alisema, “Ni hatua nyingine, uzoefu mwingine, katika maisha ya soka si kila hatua inakuwa ni kwenda mbele tu, baada ya hapo huenda akahitaji kurudi nyuma hatua tatu ili kwenda mbele tena lakini nafikiri ni haki yake, hilo linatuma ujumbe mzito kuhusu sisi ni nani pamoja na klabu hii.”
“Nilimwambia atakuwa nasi na kwamba nataka apate uzoefu wa namna mambo yanavyokuwa kuanzia hotelini, maandalizi ya mechi yanavyokuwa kati ya vijana na kwamba awe tayari, unapokuwa katika benchi ni lazima uwe tayari, kijana alichofanya ni kuniangalia usoni na kuonyesha kwamba yuko tayari.
“Maamuzi yote tuliyoyachukua na ambayo niliyachukua ni kwa ajili ya klabu, si kwa ajili yangu, si kwa ajili ya mchezaji, ni kwa sababu tunaamini ana kipaji ambacho kinahitaji kuendelezwa vizuri kwa miaka miwili au mitatu, tutaona namna tutakavyolisimamia hilo lakini kijana huyu ndiye atakayetuongoza, kimsingi si sisi,” alisema Arteta.
Kimataifa Kinda miaka 15 aweka rekodi EPL
Kinda miaka 15 aweka rekodi EPL
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
