Manchester, England
Straika wa Manchester United, Anthony Martial amewatolea uvivu makocha wake wa zamani, Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer kwa namna ambavyo hakufurahia kufanya nao kazi wakati wakiwa makocha wa timu hiyo.
Martial ambaye msimu wa 2015/16 alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo lakini baada ya Mourinho kuwa kocha wake msimu uliofuata, mchezaji huyo alijikuta katika wakati mgumu kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Alisema kwamba ingawa timu ilipata mataji chini ya Mourinho katika msimu wake wa kwanza lakini Martial anasema uwapo wa kocha huyo ulimkwaza kupata nafasi ya kuiwakilisha Ufaransa kwenye fanali za Kombe la Dunia mwaka 2018.
“Tatizo lilianzia kwenye namba ya jezi, wakati wa likizo alinitumia ujumbe akiniuliza kama nitakuwa tayari kuvaa namba 11, akaniambia hilo ni jambo kubwa kwa sababu namba hiyo ilikuwa ya mkongwe Ryan Giggs, nilimwambia namheshimu sana Giggs lakini ningependa niendelee na namba 9 yangu, lakini niliporudi likizo nilikuta jezi yangu ikiwa namba 11, mambo hayakwenda vizuri kuanzia hapo,” alisema.
“Alinidharau, alikua akinizungumzia kwenye vyombo vya habari kwa kutumia vimisamiati, kidogo kama alivyokuwa akimfanyia Karim Benzema akiwa Real Madrid, nilikuwa mfungaji bora kwenye timu nusu ya msimu akamnunua Alexis Sanchez na hapo sikuwa mwenye kucheza na hilo liliniathiri sana, ulikuwa msimu wa Kombe la Dunia na Ufaransa ikabeba taji, nami ningekuwa kwenye ile timu.”
Akizungumzia wakati wa Solskjaer, Martial alisema kwamba alilazimika kucheza akiwa na maumivu na hivyo kushindwa kucheza katika ubora wake.
“Misimu miwili iliyopita nililazimika kucheza kila wakati nikiwa majeruhi, watu hawajui hilo, sikuweza kuwa katika kiwango katika miezi minne ya COVID, Solskjaer akaniambia kwamba anataka nicheze kwa hiyo nilicheza,” alisema.
“Hali ikawa tete, nikawa mtu wa kusakamwa, kocha hakuwahi kujisumbua kuwaambia hilo waandishi wa habari, mwishowe niliumia zaidi na niliporudi nikakwama, sikuwa mwenye kucheza tena, ilinikera niliona sikutendewa haki, unaambiwa ujitoe kwa ajili ya timu lakini nyuma yake ni kusakamwa, kwangu ilikuwa hovyo, hayo ndiyo yaliyonikera, naweza kulaumiwa lakini si kwa kuwa muongo,” alisema.
Martial kwa sasa anasumbuliwa na matatizo ya misuli na kocha wake wa sasa Erik ten Hag hajaweza kusema ni lini mshambuliaji huyo atakuwa fiti na kurudi uwanjani.
Kimataifa Martial amtolea uvivu Mourinho
Martial amtolea uvivu Mourinho
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
