Barcelona, Hispania
Jumatano imekuwa nzuri kwa Robert Lewandowski, amecheza mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na jezi ya Barcelona na kufunga mabao matatu (hat trick) wakati timu hiyo ikiichapa Viktoria Plzen mabao 5-1 na kuweka rekodi ya kufunga hat trick na timu tatu tofauti.
Karamu ya mabao kwa Barca waliokuwa nyumbani ilianzia dakika ya 13 kwa bao lililofungwa na kiungo Franck Kessie na kufuatiwa na bao la Lewandowski katika dakika ya 34 akiitumia vizuri mpira uliotokana na kona lakini dakika moja kabla ya mapumziko, Viktoria walipambana na kupata bao lililofungwa kwa kichwa na Jan Sykora.
Lewandowski ambaye baada ya mechi hiyo alikabidhiwa mpira, aliipatia Barca bao la tatu katika dakika za nyongeza kabla ya timu kwenda mapumziko akiujaza mpira wavuni kwa kichwa kabla ya kuifungia timu yake bao la nne na la tatu kwake katika dakika ya 67 wakati bao la tano lilifungwa na Torres katika dakika ya 71..
Kwa mabao hayo, Lewandowski anakuwa amejiwekea rekodi ya kufunga hat trick mara sita katika Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini pia anakuwa amefanya hivyo katika timu tatu tofauti, amewahi kufanya hivyo akiwa Bayern Munich, Borussia Dortmund na sasa Barca.
Akimzungumzia Lewandowski kocha wa Barca, Xavi Hernandez alisema, “Siwezi kumpongeza kiasi cha kutosha kwa sababu tu ya hat trick, ni kwa mengi, anavyofanya kazi yake, anavyojua kuendana na kasi ya mchezo, anavyofanya mazoezi, anavyoisaidia timu, hivyo ndivyo Lewandoski alivyo.
Liverpool mambo magumu
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Liverpool timu iliyofikia fainali msimu uliopita, Jumatano haikuwa siku nzuri kwao baada ya kuchakazwa mabao 4-1 na Napoli.
Matokeo hayo ni wazi yamemvuruga kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ambaye sasa anasema anahitaji kuja na mbinu mpya za kuirudisha Liverpool katika ubora wake.
“Kila kitu kimekwenda vibaya, hilo liko wazi lakini ni kwa nini hali hii imetokea, siwezi kujibu swali hilo hapa, ngoja nitafakari, hakika kilichotukuta ni kitu kibaya lakini lazima nikipokee,” alisema Klopp.
Katika mechi hiyo, Liverpool ilizidiwa kwa kila kitu katika kipindi cha kwanza na ilikuwa kama yenye bahati kwa kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 3-0 ambapo Klopp, aliyeiwezesha Liverpool kulibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019 na kuwafikisha fainali msimu uliopita alisema kuna mambo ya kurekebishwa.
“Ni kwamba tunatakiwa kuja kivingine sisi wenyewe, kuna mapungufu mengi si katika mechi zote ila ni kwa wakati huu, jambo la kufurahisha ni kwamba tunatakiwa kufanya hivyo wakati Ligi Kuu England ikiendelea lakini pia tupo kwenye kampeni ya Ligi ya Mabingwa,” aliongeza Klopp.
Matokeo yote ya mechi za Jumatano ni kama ifuatavyo…
Ajax 4-0 Rangers
Frankfurt 0-3 Sporting
Napoli 4-1 Liverpool
Atl Madrid 2-1 FC Porto
Barcelona 5-1 Viktoria Plzen
Inter Milan 0-2 Bayern Munich
Tottenham 2-0 Marseille
Club Bruges 1-0 B Leverkusen
Matokeo ya mechi za Jumanne ni kama ifuatavyo…
Dinamo Zagreb 1-0 Chelsea
FC Red Bull 1-1 AC Milan
Celtic 0-3 Real Madrid
RB Leipzig 1-4 Shakhtar Donetsk
Borussia Dortmund 3-0 FC Copenhagen
Sevilla 0-4 Manchester City
Benfica 2-0 Maccabi Haifa
Paris Saint Germain 2-1 Juventus
Club Bruges 1-0 B Leverkusen
Kimataifa Lewandowski apiga hat trick, Liverpool hoi
Lewandowski apiga hat trick, Liverpool hoi
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
