Paris, Ufaransa
Kocha wa Paris Saint-Germain (PSG) Christophe Galtier amewaambia mastaa watatu wa timu hiyo, Lionel Messi, Kylian Mbappe na Neymar kwamba wanatakiwa kukubali kukaa benchi watake wasitake.
Galtier inaonekana hana tabia ya kuwaendekeza wachezaji mastaa na Jumamosi iliyopita alimuweka benchi Neymar ikiwa ni siku chache kabla ya mechi yao timu hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus.
Neymar aliingia uwanjani kwenye dakika ya 60 na alikuwa ni Mbappe aliyekwenda benchi kumpisha Neymar na katika hali ambayo haikutarajiwa, Mbappe hakuonekana kuchukizwa kwa namna yoyote na uamuzi huo wa Galtier.
Kati ya mastaa hao watatu, Messi ndiye aliyecheza mara nyingi lakini naye alijikuta akienda benchi katika hatua ya mwisho mwisho kwenye mechi dhidi ya Monaco na Toulouse.
Galtier, kocha aliyejiunga na timu hiyo akichukua nafasi ya Mauricio Pochettino, alisema kwamba kwake yeye ni timu kwanza na jambo hilo linaonekana kumpa mafanikio kwani katika mechi sita za PSG za Ligi 1, timu hiyo imefunga jumla ya mabao 24.
“Nimelizungumzia hilo mara mbili, mara moja kwa kila mmoja wao na mara ya pili kwa timu nzima, niliwaambia kwamba hivyo ndivyo itakavyokuwa na ni lazima tuwe na mienendo sahihi na kulikubali hilo,” alisema Galtier.
Kutokana na ratiba kuwa yenye mambo mengi na kukaribia kwa fainali za Kombe la Dunia, Galtier alisema kwamba uchaguzi uliopo ni mdogo.
“Unaweza kusema ni jambo jipya, lakini ni jukumu la kila mtu kwa sababu ya ratiba kuwa na mambo mengi, tunacheza mechi nyingi, kila baada ya siku tatu, na tena kila baada ya siku nne na hapo hapo kuna Kombe la Dunia, kila mtu ni lazima aelewe kwamba hatoweza kucheza kila mechi,” alisema.
Staa mwingine ambaye alikumbana na benchi ni Sergio Ramos katika mechi na Nantes ambapo aliingia katika dakika ya 62.
Mbappe na Neymar wamewahi kuingia katika mabishano ya nani apige penalti lakini Mbappe baada ya tukio hilo amenukuliwa akisema kwamba wana uhusiano mzuri.
“Uhusiano wetu wakati wote upo hivyo, kuna wakati tunakuwa na hasira na wakati mwingine tunakuwa na furaha, kuna wakati tunakuwa kama marafiki wakubwa na wakati mwingine huwa tunazungumza kidogo lakini mara zote tunaheshimiana,” alisema Mbappe.
“Unapokuwa na wachezaji wawili wenye mambo makubwa, matukio ya aina hii hujitokeza wakati wote lakini kikubwa tunaheshimiana, na mapenzi ya PSG yapo kwenye mioyo yetu.
Kimataifa Messi, Neymar, Mbappe waambiwa, benchi lawahusu
Messi, Neymar, Mbappe waambiwa, benchi lawahusu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
