Na mwandishi wetu
Matumaini ya Taifa Stars kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) nchini Algeria yameishia katika jiji la Kampala, Uganda Jumamosi hii baada ya timu hiyo kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Timu ya Taifa ya Uganda au Uganda Cranes.
Katika mechi hiyo wenyeji The Cranes waliandika bao lao la kwanza katika dakika ya 16 kwa mkwaju wa penalti uliojazwa wavuni na Moses Waswa na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko The Cranes wakiwa mbele.
Dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili, The Cranes waliandika bao la pili lililofungwa na Richard Basangwa kabla ya Rogers Mato kuandika bao la tatu katika dakika ya 76 na hivyo kuifanya Stars ikose tiketi ya kwenda Algeria ikiwa imetolewa kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya awali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Matokeo mabaya ya mechi ya kwanza dhidi ya The Cranes yalisababishwa kuondolewa kwa aliyekuwa kocha mkuu wa Stars, Kim Poulsen na wasaidizi wake na nafasi yake kukabidhiwa Honour Janza akisaidiwa na Mecky Maxime wakati Juma Kaseja akipewa jukumu la kuwanoa makipa wa timu hiyo.
Stars ilizianza mbio hizo kwa kuitoa timu inayotajwa kuwa ni dhaifu ya Somalia kwa jumla ya mabao 3-1 ikianza na ushindi wa bao 1-0 na ushindi wa pili wa mabao 2-1 mechi ambazo zote zilichezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na baada ya hapo ikakutana na The Cranes.
Michuano ya CHAN ambayo ilianza rasmi mwaka 2009 nchini Ivory Coast na Stars kufuzu kwa mara ya kwanza ikiwa chini ya kocha Marcio Maximo ikiwa na wachezaji Haruna Moshi ‘Boban’, Mussa Hassan Mgosi, Mrisho Ngassa, Shedrack Nsajigwa, Jerry Tegete, Salum Sued, Nadir Haroub Cannavaro, Mwinyi Kazimoto na wengineo iliishia hatua ya makundi.
Kimataifa Safari ya Stars CHAN yaishia Kampala
Safari ya Stars CHAN yaishia Kampala
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
