London, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amewataka wachezaji wa timu hiyo kuboresha kiwango, kujituma zaidi na kuwa na hamasa ya kusaka ushindi baada ya kuanza vibaya mechi tatu za mwanzo za Ligi Kuu England.
Liverpool imeianza ligi hiyo kwa sare mbili dhidi ya Fulham na Crystal Palace kabla ya kujikuta ikilala kwa mabao 2-1 mbele ya mahasimu wao Man Utd Jumatatu iliyopita na Jumamosi watakuwa nyumbani Anfield dhidi ya Bournemouth.
“Ni lazima tuboreshe soka letu haraka, tunahitaji juhudi kwa asilimia 100 kama si zaidi kidogo ya hapo, pamoja na kuwa na matamanio, ni soka la kiwango cha juu, mambo yote yako sawa, mafanikio tuliyoyapata hayakuwa rahisi, kwa hiyo kusiwe na mtu wa kutarajia mambo kuwa rahisi kwa sasa, twende pamoja,” alisema Klopp.
“Kazi yangu ni kuweka mambo sawa, nimeweza kujifunza mengi katika maisha pale mambo yanapokwenda vibaya, hiyo ni sehemu ya kazi yangu, kuwaunganisha, kutafuta namna iliyo sahihi ya kupambana pamoja kwa mara nyingine na kutoruhusu kupata tabu,” alisema.
“Tulicheza mechi hovyo dhidi ya United lakini kinachokatisha tamaa ni kwamba tulitakiwa kushinda mechi ile hasa kwa kuwa na umiliki wa asilimia 70 dhidi ya timu yenye mashambulizi ya kushitukiza,” aliongeza Klopp.
Klopp pia alipuuzia habari za kuwapo hali ya kutofautiana kati ya James Milner na Virgil van Dijk baada ya sintofahamu kuibuka baina ya wachezaji hao wawili United ilipopata bao lake la kwanza kupitia kwa Jadon Sancho.
“Ni jambo lililo wazi kila mmoja alishuhudia, mimi pia nilikuwa mchezaji mwenye mzuka enzi zangu na nilikuwa na aina hii hii ya mazungumzo uwanjani mara kwa mara kuzidi hata na marafiki zangu, sina cha kufafanua, ni mazingira ambayo mnakuwa mnajadiliana mambo uwanjani na kwa kuwa siku hizi kamera zinakuwa kibao uwanjani hapo inaonekana kama ni tatizo kubwa, si tatizo hata kidogo,” alisema Klopp.
Klopp pia alisema kwamba wachezaji wake Joel Matip, Thiago Alcantara, Curtis Jones na Diogo Jota wanaendelea vizuri japo wataikosa mechi dhidi ya Bournemouth.
Kimataifa Klopp ataka wachezaji wajitume
Klopp ataka wachezaji wajitume
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
