Na mwandishi wetu
Kusimama kwa Ligi Kuu ya NBC kumempa nafasi nzuri Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi kukiimarisha kikosi chake kuelekea michezo ijayo ya mashindano yote ambayo inawakabili.
Ligi hiyo imesimama kwa sasa kupisha mechi za timu za taifa ambapo ligi hiyo ikirejea Yanga itaumana na Azam, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kujipanga kwa timu hizo mbili.
Nabi ameeleza kuwa alichopanga kukifanyia kazi kipindi hiki ni kupandikiza mifumo ya uchezaji na kuimarisha safi ya ulinzi na ushambuliaji ambazo zimeonekana kitofanya vizuri kama linavyohitaji benchi la ufundi la mabingwa hao watetezi.
“Tutafanya mazoezi ya nguvu kuimarisha utimamu wa wachezaji sababu kabla ya ligi kuanza hatukupata muda wa kutosha kwa hiyo tukimaliza programu hiyo tutacheza mechi nyingi za kirafiki na timu za Ligi Kuu,” alisema Nabi.
Katika kukiweka sawa kikosi chake pia wamelenga maandalizi ya mchezo wao wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zolan FC ya Sudan Kusini ambapo wataanzia ugenini Septemba 6, mwaka huu.
Nabi ameeleza kuwa anajua atawakosa baadhi ya wachezaji walioitwa kwenye majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars inayojianda kucheza na Uganda kuwania kufuzu fainali za CHAN, lakini hana shaka na hilo sababu anaridhishwa na mazoezi wanayopata huko waliko.
Kocha huyo alisisitiza kwamba huu ni msimu ngumu kwao kutokana na mafanikio waliyoyapata msimu uliopita, lakini anaamini watapambana kuhakikisha wanatetea mataji yote ambayo wanayashikilia.
Yanga inashikia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi sita sawa na vinara Simba inayoongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Soka Nabi ageuza neema mapumziko ya ligi
Nabi ageuza neema mapumziko ya ligi
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
