Na mwandishi wetu
Beki wa Coastal Union, Mtenje Albano amemuomba radhi kiungo wa Yanga, Yanick Bangala kwa kumchezea mchezo usio wa kiungwana, timu hizo zilipokutana hivi karibuni kwenye mechi ya Ligi Kuu ya NBC Bara.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha na Yanga kushinda kwa mabao 2-0, Mtenje alipewa kadi ya njano baada ya tukio hilo.
Kwa lugha ya soka, wakati wanawania mpira huo nusu kwa nusu, Mtenje alinyoosha mguu kwa makusudi na kupiga hatua moja zaidi na kumkanyaga Bangala mguuni aliyekuwa anakuja kuuwania mpira huo bila tahadhari.
Mtenje amefafanua kuwa baada ya kuisha kwa mechi hiyo alimfuata Bangala na kumwomba radhi kabla ya baadaye kumpigia tena simu na kumsisitizia juu ya radhi yake hiyo na sasa yamekwisha.
“Nilimchezea Bangala mchezo usio wa kiungwana na ambao haukubaliki katika familia ya mpira, hivyo nachukua nafasi hii kuwajulisha wapenzi na wapenda mchezo huu mkubwa baada ya tukio lile nilimuomba msamaha kaka Bangala pale uwajani.
“Na baadaye pia niliongea naye kwenye simu nikirudia kumuomba radhi na yeye alinihakikishia amenisamehe kwa dhati ya moyo, kitendo ambacho kwangu kimenipa faraja sana, ama kweli wagombanao ndiyo wapatanao, hivi sasa mimi na Bangala ni marafiki,” alieleza Mtenje kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
Soka Beki Coastal amuomba radhi Bangala
Beki Coastal amuomba radhi Bangala
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
