Na mwandishi wetu, Arusha
Yanga leo imeendeleza ubabe kwa Coastal Union baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC iliyopigwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kama ambavyo Simba imeinyuka Kagera Sugar kwa ushindi kama huo jijini Dar es Salaam.
Ushindi wa Simba unakuwa na maana kubwa kwani sasa timu hiyo inashika usukani wa ligi hiyo ikiwa na pointi sita na mabao matano na haijaruhusu nyavu zake kutikiswa japo mara moja. Katika mechi ya Yanga, bao la kwanza la timu hiyo lilipatikana dakika ya nne tu ya mchezo huo mfungaji akiwa ni Benard Morrison kabla ya Fiston Mayele kuipatia timu hiyo bao la pili katika dakika ya 67 na hivyo kuifanya Yanga kupata ushindi wa tatu mfululizo dhidi ya Coastal katika kipindi kisichozidi miezi miwili.
Coastal ndiyo iliyoipa Yanga taji la Ligi Kuu ya NBC baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 na kuifanya timu hiyo kutangazwa kinara wa ligi hiyo msimu wa 2021/22 mwishoni mwa mwezi Juni na baada ya hapo Yanga ikaichapa tena Coastal kwa penalti 4-1 katika mechi ya fainali ya Kombe la FA.
Katika mechi hiyo ya FA iliyopigwa Julai 2 kwenye dimba hilo hilo la Sheikh Amri Abeid, timu hizo kwanza zilimaliza dakika 90 za kawaida kwa sare ya mabao 2-2 na zikatoka tena sare katika dakika 30 za nyongeza na ndipo zilipopigiana penalti na Yanga kuibuka kidedea.
Katika mechi ya leo, mpachika mabao ya Yanga, Mayele alianzia benchi na kuingia katika dakika ya 54 akichukua nafasi ya Makambo, mabadiliko ambayo yalizaa bao dakika 13 baadaye, Mayele alipofunga bao la kichwa kwa mpira ulioanzia kwa kona ya Morison na kumkuta Djuma Shaaban aliyemuunganisha Mayele kwa kichwa na Mayele bila ajizi akaujaza wavuni na kuanza kushangilia kwa staili yake maarufu ya kutetema iliyopokewa vizuri na mashabiki wa Yanga waliofika Sheikh Amri Abeid.
Coastal katika mechi hiyo licha ya kupambana lakini haikuwa na madhara makubwa kwa Yanga badala yake ilifanya mashambulizi machache, mojawapo ilikuwa ni katika dakika ya 54 Maabad Maulid Maabad alipoambaa na mpira upande wa kushoto na kulikaribia lango la Yanga lakini shuti alilopiga akiwa karibu na lango halikuwa na madhara yoyote.
Huo unakuwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa Yanga katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu baada ya kuilaza Polisi Tanzania mabao 2-1 katika mechi yao ya kwanza wakati kwa Coastal hiyo inakuwa mechi yao ya kwanza kupoteza, ilianza ligi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC.
Nao Simba walineemeka na mabao ya Mosses Phiri katika dakika ya 42 na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Simba ikiwa mbele kabla ya kuongeza bao la pili dakika nane kabla ya mpira kumalizika mfungaji akiwa Dejan Georgijevic au Mzungu kama alivyoeleka mbele ya mashabiki wa Simba.
Kama ilivyo kwa mahasimu wao, Yanga, Simba nao huo unakuwa ushindi mwingine wa pili mfululizo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Geita.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochewa leo, Tanzania Prisons iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji, hiyo ikiwa ni mechi ya pili kwa Dodoma kushindwa, timu hiyo iliianza ligi kwa kufungwa mabao 3-1 na Mbeya City kama ilivyo Prisons iliyoianza ligi kwa kufungwa bao 1-0 na Singida Big Stars.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili hii kwa mechi zifuatazo
Mtibwa vs Ruvu Shooting
Azam vs Geita Gold
Singida Big vs Mbeya City.
Matokeo ya mechi za wiki iliyopita ni kama ifuatavyo…
Namungo-2-2 Mtibwa Sugar
Ihefu 0-1 Ruvu Shooting
Singida Big 1-0 Prisons
Azam 2-1 Kagera Sugar
Simba 3-0 Geita
Coastal Union-1-0 KMC
Dodoma Jiji 1-3 Mbeya City
Polisi Tanzania-1-2 Yanga
Soka Yanga. Simba zatakata Ligi Kuu NBC
Yanga. Simba zatakata Ligi Kuu NBC
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
