Manchester, England
Chris Daw, wakili wa mwanasoka wa zamani wa Man Utd, Ryan Giggs ameiambia Mahakama ya Manchester kuwa madai ya mpenzi wa zamani wa mwanasoka huyo, Kate Greville kwamba michubuko aliyonayo ilitokana na kupigwa na Giggs ni uwongo mtupu.
Giggs amejikuta katika wakati mgumu akituhumiwa kumshambulia na kumdhalilisha Kate na mdogo wake Emma Greville pamoja na makosa mengine tuhuma ambazo amezikana ingawa amelazimika kung’atuka kuinoa timu ya Taifa ya Wales inayojiandaa kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
Kate hata hivyo wakati akihojiwa na wakili wa Giggs Jumatano hii alijikuta akiangua kilio alipokuwa akijibu maswali hasa kuhusu madai yake kwamba alipigwa na Giggs mwaka 2017 wakati wawili hao wakiwa kwenye chumba cha hoteli moja huko Dubai.
Maswali hayo yalitokana na madai ya Kate alipoiambia mahakama kwamba Giggs alimkaba shingo na kumburuta hadi kwenye varanda baada ya kutokea mzozo baina yao sababu ikiwa ni hisia alizokuwa nazo Kate kwamba Giggs alikuwa akiwasiliana na mwanamke mwingine kupitia ujumbe mfupi wa simu ingawa Daw alimtetea Giggs akidai kwamba ujumbe huo alikuwa akimtumia binti yake
Baada ya hapo, Daw alimuuliza Kate kuhusu michubuko ambayo alidai ilitokana na kipigo lakini wakili huyo alikumbushia taarifa ya awali ya Kate akidaiwa kumwambia mshirika wake katika biashara, Elsa Roodt kwamba michubuko hiyo ilitokana na ‘vurugu za mambo ya mapenzi’.
Akijibu hoja hiyo, Kate alisema kwamba aliogopa kumwambia Elsa kwa kuwa alijiona aliyedhalilishwa na hakutaka kukiri ukweli huo.
Akiyachambua majibu hayo ya Kate, Daw alisema, “Kwa hiyo yote hayo ya kuwa ni majeraha ya fujo za kwenye mapenzi ni uwongo, yaani si kweli kwamba ni yale mambo ambayo wote mliyafurahia.”
Baada ya hapo wakili huyo aliizungumzia picha ambayo Kate alijipiga akiwa mbele ya kioo na kumtumia Giggs siku kadhaa baada ya madai ya kushambuliwa na wakili huyo kuhoji kama kuna alama yoyote ya michubuko. “Hapana hiyo picha haijatoka vizuri,” alisema Kate akijibu hoja ya wakili huyo.
“Kwa hiyo suala zima la michubuko kwenye ‘vurugu wakati wa mapenzi’ ni ujanja ujanja usio na mantiki. Ukweli ni kwamba mara kwa mara umekuwa ukipata michubuko kutokana na mambo ya mapenzi.” Kate alijibu swali hilo akisema kwamba hakumbuki kitu hicho.
Baada ya hapo Daw alisoma ujumbe ambao Giggs na Kate walikuwa wakitumiana ambako Kate alianza kwa kumwambia Giggs, “Nakutaka ile mbaya, nataka fujo zako.” Giggs naye akajibu, “Kweli, naogopa kukuumiza.” Kate akamjibu, “Nataka kuumizwa kidogo, si katika namna ya hovyo, nataka unishtue na na uni-surprise. “Katika majibu yake Giggs akamwambia, “Hiyo sawa.” Kabla ya Kate naye kumjibu, “sawa tutaipata furaha katika hilo.
Akijitetea kuhusu suala hilo, Kate alisema kwamba Giggs alikuwa akimwambia fanya jambo fulani ilikuwa ni lazima afanye vinginevyo angejikuta katika wakati mgumu.
Alisema kwamba amefanya tafiti kuhusu tabia za Giggs na anaamini kwamba ana matatizo na kwamba alichokuwa akikutana nacho kwa Giggs ni sawa kabisa na kile alichokuwa akikifanyia tafiti.
Alipoulizwa na Daw kama Giggs alikuwa mtu wa vurugu kwake kila saa, Kate alisema kwamba haikuwa kila saa bali alikuwa na tabia hizo mara kwa mara, “Hakuwa na matukio ya ukorofi kila saa lakini kuna wakati mahusiano yetu yalipitia katika vurugu,” alifafanua Kate.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, Kate alitoa kauli ambayo iliacha maswali aliposema kwamba azma ya kufungua kesi hiyo si kutaka malipo ya fidia.
t
