Na Hassan Kingu
Desemba 2012 kwenye michuano ya Cecafa, Kilimanjaro Stars ikiwa chini ya kocha Kim Poulsen iliibugiza Somalia mabao 7-0. Jumamosi iliyopita Taifa Stars ambayo sehemu kubwa ya wachezaji wake ni wale wa Kili Stars ilipata ushindi mdogo wa bao 1-0 na jana ikapata ushindi wa mabao 2-1 kocha akiwa ni yule yule Kim.
Matokeo haya yanatosha kutufanya tuwe na maswali ya kutufikirisha kwa kina, nini kimelipata soka letu, je ni Somalia wamepiga hatua kutoka kufungwa mabao 7-0 hadi kupambana na kufungwa bao 1-0 na baadaye 2-1 katika mechi ya marudiano? Je ni soka la Tanzania limedumaa wakati la Somalia likianza kupiga hatua?
Tunahitaji kufikiri kwa kina kwa sababu kwa kipindi kirefu Somalia imekuwa ikionekana ni kibonde wa Tanzania na majirani zake katika ukanda wa Cecafa, wakati pekee ambao Somalia ilionekana kufanya maajabu ilikuwa ni katika michuano ya Cecafa 2008/09 ilipoichapa Kilimanjaro Stars bao 1-0, hii ilionekana kuwa ni aibu kwa Tanzania kama ambavyo msimu wa 2007/0, Kili Stars ilipata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Somalia na kuonekana imepata ushindi mwembamba.
Tofauti na hapo kwa kipindi cha miaka takriban 25 iliyopita Somalia imekuwa kibonde, mwaka 2015/16 kwenye michuano ya Cecafa ilipigwa na Kilimanjaro Stars mabao 4-0, mwaka 2010/11 ikapigwa mabao 3-0. Somalia katika michuano ya Cecafa ilikuwa kama daraja la timu nyingine kusonga mbele au washambuliaji kuitumia kuwa wafungaji bora katika michuano ya Cecafa.
Mfano ni Mrisho Ngassa katika michuano ya Cecafa mwaka 2012 nchini Uganda alikuwa mmoja wa washambuliaji watatu waliofunga mabao matano kila mmoja, manne kati ya hayo aliyapata katika mechi dhidi ya Somalia. Mwingine alikuwa ni John Bocco ambaye mawili kati ya mabao yake matano aliyafunga katika mechi na Somalia.
Hali hiyo ndiyo inayoibua maswali ya kutufikirisha kwa kina kwamba nini kinaendelea kwenye soka la Somalia, je matokeo ya hivi karibuni ni bahati tu imewaangukia? Je Stars waliwadharau Somalia au ni Somalia wameanza kubadilika?
Ukichambua ushindi wa mabao 7-0, 4-0 na 3-0 ambao Tanzania imekuwa ikiupata dhidi ya Somalia halafu ukatokea ushindi wa bao 1-0 au 2-1, unajikuta ikiwaza mengi lakini pia unaweza kuiona Somalia imepiga hatua na hivyo inahitaji kupongezwa.
Unapozungumzia kushindwa kwa timu, mara nyingi mhanga wa kwanza kurushiwa lawama anakuwa kocha lakini leo hii nimeamua kuizungumzia timu iliyoshinda nikitaka kuwafikirisha mashabiki wa soka kuhusu ushindi uliopatikana dhidi ya timu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikionekana ni kibonde.
Ningependa badala ya kumfikiria kocha peke yake tulifikirie soka letu kwa mapana yake kwamba hali imekuwaje hadi kujikuta timu inapata ushindi mwembamba dhidi ya timu ambayo imekuwa ikitajwa kuwa ndiye kibonde.
Wakati fulani huko nyuma wakati Somalia ikiwa yenye kufungwa kuna ambao waliwahi kudai kwamba timu hiyo hata maandalizi yao ni ya kawaida au ya kuungaunga, si ya timu inayokwenda kushindana na ilidaiwa kwamba mara nyingi timu hiyo inaandaliwa katika jiji la Nairobi, Kenya kutokana na mazingira magumu ya kiusalama nchini kwao.
Kwa mazingira ya aina hiyo haishangazi kuona ikiwa kibonde lakini inashitusha kidogo timu ya aina hiyo ambayo ingetarajiwa ifungwe mabao mengi inafungwa mabao machache na kama bado iko katika mazingira magumu na maandalizi ya kuungaunga ama hakika kuna kila sababu ya kuwapongeza wachezaji wa Somalia kwa matokeo waliyoyapata.
Kulifikiria soka letu kusiishie kwa Somalia tu bali tuna wajibu pia wa kujifikirisha kupitia soko la nchi nyingine, mfano Comoro na maendeleo ya timu yao ya Taifa ambayo huko nyuma ilikuwa haitishi lakini kwa sasa ukiizungumzia Comoro kwenye soka unazungumzia mambo makubwa yanayoanza kuonekana. Tujifikirishe pia kupitia soka lao huku tukitafakari matatizo la soka letu kwa mapana yake badala ya kumuangalia mtu mmoja, mmoja.
Kimataifa Tuipongeze Somalia kwa kufungwa na Stars
Tuipongeze Somalia kwa kufungwa na Stars
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
