Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa klabu ya PSG, Neymar amesema kwamba anapenda kubaki katika klabu hiyo ya jijini Paris lakini hana uhakika klabu hiyo ina mpango gani kuhusu majaliwa yake.
Awali PSG waliwahi kudai kwamba wako tayari kumruhusu mchezaji huyo aondoke katika kipindi hiki cha kiangazi huku Chelsea na Man City zikidaiwa kuwa tayari kumsajili ingawa baadaye City walijitoa katika mpango huo.
Neymar, 30 ambaye amecheza kipindi cha pili katika mechi ya maandalizi ya msimu dhidi ya Urawa Red Diamond Jumamosi hii na PSG kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, baada ya mechi hiyo aliamua kuwa wazi kuhusu mipango yake ya baadaye.
“Bado nina shauku ya kubaki katika klabu hii, hadi sasa klabu haijaniambia lolote kwa hiyo sijui mipango yao kwangu,” alisema Neymar mara baada ya mechi hiyo.
Kauli ya Neymar imekuja baada ya kocha mpya wa PSG, Christophe Galtier kunukuliwa akisema baada ya mechi hiyo kwamba hana uhakika kama mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil ataendelea kuwa katika klabu hiyo.
“Neymar amekuwa akifanya juhudi tangu kuanza kwa msimu, pia kwangu anaonekana kuwa mwingi wa furaha na yuko fiti, nilizungumza kuhusu mambo yake kwenye mkutano na waandishi wa habari,” alisema Galtier.
“Kitakachojitokeza siku chache zijazo mwishoni mwa kipindi cha usajili sikijui, sijafanya mazungumzo naye ya ana kwa ana kuhusu jambo hilo lakini kwangu haonekani kama mtu ambaye hajatulia kuhusu kile watu wanachomzungumzia au hali ilivyo katika klabu yake, anafanya mazoezi na kuyafurahia,” aliongeza Galtier.
Kwa upande wake Neymar naye alisema, “ukweli ni kwamba sina chochote cha kumthibitishia yeyote, watu wanazunguma kwa sababu hawana jambo jingine la kufanya, wananijua mimi, wanajua jinsi ninavyocheza, sina cha kuthibitisha, napenda kucheza soka, na nina furaha.”
Kimataifa Neymar: Siijui hatma yangu PSG
Neymar: Siijui hatma yangu PSG
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
